Mkuu wa mkoa wa Arusha ,CPA Amos Makalla akizindua sehemu maalumu ya kupokelea wagonjwa wa dharura pamoja na magonjwa yasiyoambukiza katika hospitali ya ALMC (Selian ) iliyopo jijini hapa.

…….
Na Happy Lazaro, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha ,CPA Amos Makalla amewataka wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza yanayotolewa na Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI )katika hospitali ya ALMC (Selian ) jijini Arusha .
CPA Makalla ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizindua sehemu maalumu ya kupokelea wagonjwa wa dharura pamoja na magonjwa yasiyoambukiza katika hospitali ya ALMC (Selian ) iliyopo jijini hapa .
CPA Makalla amesema kuwa ,kitendo cha wananchi kujitokeza mapema kupima afya zao kinasaidia kuweza kugundua tatizo linalowasumbua ili waweze kupata tiba mapema kuliko kusubiri hadi tatizo linakuwa sugu ambapo inakuwa ni changamoto katika matiababu.
“Fursa hii mliyoipata ni muhimu sana na naombeni muitumie vizuri kwani wananchi wengi walitamani kambi hii iwepo.katika maeneo yao lakini haikuwezekana lakini nyie mliopata fursa hii hakikisheni mnaitumia kikamilifu .amesisitiza
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha kuwa wanajiunga na bima ya afya kwa wote ili waweze kupata vipimo,matibabu,na dawa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Aidha Sehemu hiyo maalumu ya kupokelea wagonjwa hao imekarabatiwa na kuweka vifaa tiba na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo ukarabati pamoja na vifaa tiba umegharimu kiasi cha shs 200 milioni .
CPA Makalla aliwapongeza wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo yanayotolewa na Tasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete ambayo imeweka kambi ya matibabu hospitalini hapo .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dokta Peter Kisenge amesema kuwa , Taasisi hiyo imekwisha kufungua vituo sita katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo kituo hiki.cha hapa Arusha ambacho kitahudumia mikoa ya kaskazini na mikoa jirani .
Dkt Kisenge amesema kuwa , kambi hiyo ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ilianza desemba 29 na inatarajiwa kifikia tamati januari 9, na kusema kuwa hadi sasa zaidi ya wagonjwa 1,200 wameshahudumiwa na walioonekana na tatizo kubwa walipewa rufaa ya kwenda makuu ya Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, mwitikio wa wananchi ni mkubwa hali inayoonyesha kuwa wananch9 wengi wanakabiliwa na tatizo la moyo na kuwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa siku hizo chache zilizobakia .
“Bado tatizo la magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ni tishio kubwa kwa uhai wa mwanadamu hivyo umefika wakati sasa kwa wananchi kuchunguza afya zao mapema ili kuweza kutambua afya zao badala ya kusubiri hadi dalili za ugonjwa husika kujitokeza kitendo ambacho kinakuwa ni changamoto kwenye suala la matibabu .”amesema Dkt Kisenge .
Aidha ameshukuru hospitali hiyo ya ALMC (Selian) inayomilikiwa na kanisa la Kiinjili la.kilutheri Tanzania (KKKT) pamoja na uongozi wa kanisa hilo kwa kuwakubalia kuweka kituo cha kutoa huduma ya matibabu ya moyo katika hospitali hiyo kwani lengo la JKCI ni kutaka kuona wananchi hawapotezi maisha yao kwa tatizo la moyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ngarenaro, Abdulaziz Chande (Dogo Janja) amemshukuru Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha JKCI ili kuweza kuja kutoa huduma hiyo kwa siku zote hizo kwa wananchi wa Arusha na mikoa ya jirani.
“Mimi.nina mfano ulio hai baba yangu mzazi anasumbuliwa na tatizo la moyo na ilikuwa nikitakiwa kumpeleka jijini Dar es Salaam mara mbili kwa mwezi ,lakini kufunguliwa kwa kituo hiki mkoani Arusha kimeleta faraja sio kwangu tu ila kwa wananchi wote wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo kwani imewapunguzia gharama za kwenda kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam. “amesema Dogojanja.
Kwa upande wake Mwananchi aliyenufaika na huduma hiyo Fausta Mwacha ameipongeza Taasisi hiyo kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam hali ambayo ilikuwa changamoto kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.



