Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Media, Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki ya ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha wanapata elimu bila kubaguliwa, hivyo amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto hao na badala yake kuwapeleka shuleni.
Profesa Mkenda ameyasema hayo January 5, 2026 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi na ugawaji wa magari pamoja na vifaa vya kidijitali vya kielimu na saidizi kwa walimu wakufunzi na walimu tarajali wenye ulemavu nchini, vyenye thamani ya Shilingi bilioni 6.2.
Amesema kuwa Serikali imetunga sera ya elimu inayowezesha watoto wenye changamoto kubwa kufundishwa majumbani kupitia walimu maalum, huku kwa wale wanaohitaji wasaidizi wawapo shuleni, Serikali ikiahidi kugharamia malipo ya wasaidizi hao ili watoto wenye ulemavu wasikose haki yao ya kupata elimu.
Aidha amebainisha kuwa sera ya elimu inasisitiza upatikanaji wa elimu kwa kila mwanafunzi mwenye mahitaji maalum kwa misingi ya haki, utu na usawa, akisisitiza kuwa hakuna mtoto anayepaswa kunyimwa elimu kwa sababu ya ulemavu alionao.
Amesema kuwa awali wanafunzi wenye mahitaji maalum walikuwa wanatengwa na kuwekwa kwenye vitengo maalum bila kuchanganyika na wanafunzi wengine, hali ambayo Serikali imeiamua kuiondoa kwa kuanzisha mfumo wa elimu jumuishi unaowawezesha wanafunzi wenye ulemavu kusoma pamoja na wenzao wasiokuwa na ulemavu.
Amebainisha kuwa kupitia elimu jumuishi, wanafunzi hao wanapatiwa vifaa saidizi kama vile vya kusikia, kuona na kutembea, huku wasioona wakipatiwa vitabu vya maandishi ya nukta nundu, hatua inayowawezesha kufanya vizuri zaidi kitaaluma na kujiona sawa na wanafunzi wengine.
Aidha amesema kuwa Serikali imetoa maelekezo ya vitabu vyote kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita kuchapishwa kwa maandishi ya nukta nundu ili kuwaondolea vikwazo wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amewataka wadhibiti ubora wa elimu nchini kufuatilia na kubaini changamoto zote zilizopo katika shule za halmashauri zao na kuzitafutia ufumbuzi mapema kabla hazijasambazwa mitandaoni kupitia picha au taarifa mbalimbali.
Amesema kuwa wadhibiti ubora wa elimu wanapaswa kuwasilisha changamoto hizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri husika na kuziwasilisha Wizara ya Elimu, huku taarifa hizo pia zikifika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya utekelezaji.
Amebainisha kuwa hali ya wanafunzi na walimu kutumia choo kimoja katika baadhi ya shule ni uzembe wa viongozi wa halmashauri, akisisitiza kuwa hakuna halmashauri isiyo na uwezo wa kujenga miundombinu ya msingi kama vyoo isipokuwa pale mapato yanapokuwa sifuri.
Amesema kuwa endapo wadhibiti ubora wa elimu watakuwa wanazifahamu changamoto za shule mapema, hata zikisambazwa mitandaoni, watakuwa na majibu ya kutoa kwa wananchi kwa kuwa wanajua chanzo cha changamoto hizo.
Waziri huyo pia amewataka wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kuwafikisha watoto hao katika ofisi za Serikali au kwa maofisa husika ili waweze kusaidiwa kupata elimu, akisema kuwa Serikali ipo tayari kugharamia masomo yao.
Aidha amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili kuhakikisha elimu jumuishi inatolewa kwa makundi yote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Pia amewaagiza wadhibiti ubora wa elimu nchini kutembelea kaya kwa kaya ili kuwabaini watoto wote wenye ulemavu na kuhakikisha wanaandikishwa na kuanza masomo.




