Klabu ya Manchester United imemfuta kazi meneja Ruben Amorim kama kocha mkuu wa klabu hiyo, kufuatia msururu wa matokeo yasiyoridhisha katika kipindi cha miezi 14 tangu achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Mashetani Wekundu muda mfupi uliopita imeeleza kuwa kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Darren Fletcher, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi, ameteuliwa kuwa kocha wa muda, na anatarajiwa kuiongoza timu dhidi ya Burnley siku ya Jumatano.
“Wakati Manchester United ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, uongozi wa klabu umefanya uamuzi huu kwa ‘kishingo upande’ baada ya kuona kuwa ni wakati muafaka wa kufanya mabadiliko. Hatua hii inalenga kuipa timu fursa bora zaidi ya kumaliza katika nafasi za juu zaidi kwenye msimamo wa ligi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia ripoti za kuongezeka kwa mvutano kati ya bodi ya Manchester United na Ruben Amorim kuhusu bajeti ya usajili, huku uhusiano kati ya Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo, Jason Wilcox, na Amorim ukielezwa kudorora.



