NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

THE Desk & Chair Foundation katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa vifaa vya shule miongoni mwa watoto wanaotoka katika familia duni kiuchumi,imewapatia vifaa vya elimu wanafunzi 1,000 wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza.

Msaada huo umetolewa leo, jijini Mwanza, ambapo Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Alhaji Dk. Sibtain Meghjee, alikabidhi vifaa hivyo kwa baadhi ya wanafunzi walionufaika.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Dk. Meghjee alisema licha ya serikali kutoa elimu bila malipo, bado baadhi ya wanafunzi wanakabiliwa na changamoto ya kukosa madaftari, sare, viatu na mabegi kutokana na kipato duni cha wazazi na walezi wao.

Alisema kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu, wanafunzi 1,000 wanaoendelea na masomo pamoja na wanaoanza masomo watanufaika, ili kuwapa mazingira rafiki ya kujifunzia na kuongeza ari ya masomo.

Dk. Meghjee aliishauri serikali kupunguza au kuondoa kodi kwenye vifaa vya elimu ili taasisi hiyo iweze kuwahudumia wanafunzi wengi zaidi, akibainisha kwa zaidi ya miaka 10, imekuwa ikitoa huduma kwa jamii bila kubagua kupitia kauli mbiu ya “Tupo Pamoja, Iwe Dhiki Iwe Faraja”.

Aliishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fursa kwa taasisi hiyo kutoa mchango wake kusaidia kuboresha sekta ya elimu na kuhakiki watoto wanpata haki yao ya elimu.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi walionufaika waliishukuru taasisi hiyo na kuiomba serikali kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kusaidia watoto wenye ulemavu wanaotoka katika familia zenye changamoto za ulemavu wakiwemo wa viungo kupata vifaa vya shule na haki ya elimu.

Mkazi wa Igombe wilayani Ilemela, Emmanuel Daud, alisema hali yake ya ulemavu na kipato kidogo kinachotokana na kilimo cha kujikimu vinamfanya ashindwe kumudu gharama za vifaa vya shule kwa watoto wake, hivyo akaomba serikali iangalie kundi hilo kwa jicho la huruma.

Pia, mkazi wa Pasiansi, Manispaa ya Ilemela, Baraka Obwele mwenye ulemavu wa miguu, alisema serikali iwaangalie walemavu pamoja na watoto wao kwa wapate haki ya elimu watimize ndoto zao.

“Nimshukuru Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation kwa moyo wake wa kusaidia jamii, ameendele kuwawezesha watoto vifaa vya elimu, nina watoto watatu na hapa amenisaidia mmoja. Serikali sisemi imeshindwa la, ituangalie walemevu watoto wetu wpate elimu sawa na wengine,”alisema.

Kwa upande wao wanafunzi walionufaika akiwemo Mariam Said wa Mlimani Sekondari, Latifa Ramadhan wa Ibungilo Sekondari na Mwanaisha Hassan wa Shule ya Msingi Sahara, walisema msaada huo umeongeza morali na motisha ya kusoma kwa bidii.

 “Hali duni ya kiuchumi imekuwa kikwazo kwa baadhi ya wazazi kumudu gharama za kununua vifaa vya shule kwa ajili ya watoto wao, licha ya kuwa wana mwamkoa wa elimu.Serikali irejeshe utaratibu wa zamani madaftari yapatikane shuleni, wazazi wabaki na jukumu la kununua sare na viatu,”alishauri Mariam.

Jumla ya shilingi milioni 15 zilitumika kununua katoni 354 sawa na madaftari zaidi ya 5,500 pamoja na mabegi 300, ambapo awamu ya kwanza wanafunzi 1,000 wamenufaika na awamu ya pili ya msaada huo inatarajiwa kutolewamwishoni mwa wiki ijayo.