Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akizungumza kwenye kambi hiyo jijini Arusha leo
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude,amewataka wananchi kujiunga na bima ya afya mapema ili kuepuka mzigo wa kifedha unaoweza kutokea kutokana na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza .
Ameyasema hayo leo kwenye Kambi ya Uchunguzi na Matibabu ya Magonjwa ya Moyo inayoendelea katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) .
, Mkude amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza, kama vile magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kisukari, ni tishio kubwa kwa afya ya jamii,hivyo wananchi hawana budi kujijengea tabia ya kwenda kupima afya zao mara kwa mara .
Mkude amesema kuwa wilaya hiyo imeanzisha mpango wa mafunzo ya uhamasishaji kuhusu afya katika ngazi za wilaya, kata, na mitaa, jambo ambalo litasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya afya na kinga za magonjwa haya.
“Nawaombeni sana muone umuhimu wa kuendelea na uhamasishaji kuhusu afya katika jamii, ili kuongeza uelewa kuhusu kinga na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza. “amesema Mkude.
Aidha amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha na maeneo jirani kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kujiunga na Bima ya Afya kwa wote ili kufanikisha lengo la afya bora kwa kila Mtanzania.
Aidha amesema kuwa ,kuna umuhimu mkubwa wa bima ya afya, kwani inalinda familia, inaleta utulivu kifedha, na inahakikisha huduma za matibabu zinapatikana kwa wakati.
Amepongeza serikali kwa kuimarisha huduma za afya karibu na wananchi kupitia programu ya Tiba Mkoba, ambayo imepunguza gharama za matibabu na kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi.
Mkude alifafanua kuwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa magonjwa ya moyo ni chanzo kikuu cha vifo duniani, na Mkoa wa Arusha umeathirika kwa kiwango kikubwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Amewahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya mapema ili kuepuka mzigo wa kifedha unaoweza kutokea kutokana na matibabu ya magonjwa haya.
Aidha, alitoa taarifa ya mafanikio ya kambi hiyo, ambapo zaidi ya 1000 ya wananchi, wakiwemo watu wazima na watoto, walipatiwa huduma. Katika kipindi hicho, wagonjwa 53 walithaminika kwa upasuaji wa moyo, na wengine 45 walipewa rufaa kwenda JKCI Dar es Salaam.
Kambi hiyo itaendelea hadi Januari 9, 2026, na huku Mkude akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizi muhimu.
Kwa upande wake Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), alithibitisha kuwa zoezi linaendelea vyema na wananchi wengi wamejitokeza kupata huduma.
Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa kambi hiyo, kumekuwapo na ongezeko kubwa la watu wanaojitokeza kwa uchunguzi, jambo linalothibitisha kuwa wananchi wanahitaji huduma za matibabu ya moyo kwa karibu.
Dkt. Kisenge amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watu kuendelea kuchunguzwa afya zao mara kwa mara, kwani kugundua matatizo mapema kunasaidia kupunguza madhara ya magonjwa ya moyo.
Dkt. Kisenge pia ameongeza kuwa ushirikiano kati ya JKCI na ALMC ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya, hasa katika mkoa wa Arusha ambao ni kitovu cha utalii na unahitaji huduma bora za afya kwa wananchi na wageni. Alisisitiza kuwa lengo la taasisi yake ni kuhakikisha huduma za kibingwa za moyo zinapatikana kwa urahisi, na kuhamasisha wananchi kutumia fursa za kambi hizi kama sehemu ya kujitambua na kujali afya zao.




