Na. Meleka Kulwa -Fullshangwe Media
AGADIR, MOROCCO – Beki wa kulia wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Khuliso Mudau, amepinga uamuzi wa penati uliotolewa kwa Misri katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, akisema timu yake haikuwa na bahati licha ya kutawala sehemu kubwa ya mchezo.
Afrika Kusini ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Misri katika mchezo uliochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Stade Adrar, Agadir. Bao pekee la mchezo lilifungwa na Mohamed Salah dakika ya 45 kwa mkwaju wa penalti, baada ya kuonekana kuguswa usoni na Mudau ndani ya eneo la hatari.
Mudau, anayeichezea klabu ya Mamelodi Sundowns, amesema hakuona sababu ya kutolewa kwa penalti hiyo.
“Sidhani kama ilikuwa penati kwa Misri. Mwamuzi alitoa uamuzi wake na hakuna tunachoweza kufanya. Tunapaswa kuelekeza mawazo yetu kwenye mchezo unaofuata,” amesema Mudau akizungumza na Flashscore.
Ameongeza kuwa Bafana Bafana walikosa bahati licha ya kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga.
“Hatukuwa na bahati. Tulifanya kila kitu ili kufunga lakini haikuwezekana. Tunapaswa kuzingatia mchezo unaofuata. Kuna mambo chanya ya kujifunza, kila mmoja alikuwa tayari kuisaidia timu,” amesema.
“Tulipoteza nafasi nyingi. Tukihakikisha tunatumia nafasi zetu, tutaimarika zaidi kama timu.”
Mchezo huo pia uliibua mjadala mwishoni baada ya Afrika Kusini kudai penati kufuatia mpira kuonekana kugusa mkono wa mchezaji wa Misri ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, baada ya mapitio ya VAR, mwamuzi alikataa kutoa penati hiyo.
Kocha wa Afrika Kusini, Hugo Broos, amesema hata mshambuliaji wa Misri, Mohamed Salah, alishangazwa na uamuzi wa penalti.
“Hata Salah aliniambia baada ya mchezo kuwa alishangaa kuwa ilikuwa penati,” amesema Broos.
“Katika kikao cha kabla ya mashindano waliweka wazi kuwa mkono ukiwa mbali na mwili ni penati, baadaye wakasema ni mkono wa kujisaidia. Mkono wake ulikuwa umeachana na mwili na mpira ukaugusa.”
Nahodha wa Bafana Bafana, Ronwen Williams, amesema timu yake imeathiriwa na maamuzi ya waamuzi.
“Tumesikitishwa. Lengo letu lilikuwa kushinda au kupata angalau pointi moja. Tunahisi tumetendewa isivyo haki kwa maamuzi yaliyotolewa uwanjani,” amesema Williams.
Kwa upande wake, kiungo wa Afrika Kusini, Thalente Mbatha, amesema timu hiyo ilistahili kupewa penalti.
“Tuliamini ilikuwa faulo au penati. Mwamuzi alikagua VAR, lakini uamuzi wake ni wa mwisho. Ni lazima turudi tukiwa imara zaidi kwenye mchezo unaofuata,” amesema Mbatha.
Afrika Kusini sasa inajiandaa kuikabili Zimbabwe katika mchezo wa mwisho wa Kundi B, ikihitaji angalau sare moja ili kufuzu hatua ya 16 bora ya AFCON 2025.
CHANZO: Goal.com




