Maafisa wa Tume ya Uchaguzi wanaandaa vituo vya kupigia kura ndani ya shule kabla ya uchaguzi mkuu, katika Kata ya Thingangyun, Yangon, Myanmar, Desemba 27, 2025.
Maafisa wa Tume ya Uchaguzi wanaandaa vituo vya kupigia kura ndani ya shule kabla ya uchaguzi mkuu, katika Kata ya Thingangyun, Yangon, Myanmar, Desemba 27, 2025.
Muonekano wa kituo cha kupigia kura kabla ya uchaguzi mkuu, katika Kata ya Thingangyun, Yangon, Myanmar, Desemba 27, 2025.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Media
Watu wa Myanmar wanaendelea kupiga kura katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaofanyika kwa awamu tatu, kuanzia Jumapili ya Desemba 28,2025, wakati taifa hilo likikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na hali ya kisiasa isiyo imara.
Uchaguzi huu ni wa kwanza kufanyika tangu jeshi lilipotngazwa madarakani kwa mapinduzi mwaka 2021, na serikali ya kijeshi ikisema uchaguzi huo ni fursa ya kuanzisha upya mchakato wa kisiasa na kiuchumi katika taifa hilo lililo maskini.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa, baadhi ya nchi za Magharibi na makundi ya haki za binadamu wamekosoa uchaguzi huu kwa kusema Taifa halina uhuru, haki wala uhalali kwani vyama vinavyopingana na jeshi havikupewa nafasi ya kushiriki.
Aung San Suu Kyi, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na aliyepinduliwa na jeshi miezi michache baada ya chama chake cha National League for Democracy kushinda kwa wingi uchaguzi wa mwaka 2020, bado yuko gerezani na chama chake kimefutwa.
Kiongozi wa jeshi, Jenerali Min Aung Hlaing, aliyevaa mavazi ya kiraia, alipiga kura katika mji mkuu Naypyitaw akiwa na ulinzi mkali na baadaye kuonyesha kidole kilichochomwa wino kama ishara ya kupiga kura.
Alipohojiwa kama anataka kuwa rais, alijibu kuwa si kiongozi wa chama chochote cha siasa na kwamba nafasi ya urais itachaguliwa bungeni.
Uchaguzi unaendelea katika miji mikubwa ya Yangon na Mandalay, ingawa jeshi halina udhibiti wa maeneo yote kutokana na mapigano yanayoendelea nchini kote.
Chama kinachounga mkono jeshi, Union Solidarity and Development Party (USDP), kinatarajiwa kushinda uchaguzi huu kwa kuongoza wagombea wengi ikilinganishwa na wapinzani waliopunguzwa sana.
Wakati wa uchaguzi, mashirika ya habari ya serikali yameripoti kuwasili kwa waangalizi kutoka nchi kama Urusi, China, Belarus, Kazakhstan, Cambodia, Vietnam, Nicaragua na India.
Hata hivyo, mzozo na mapigano vinaendelea kuathiri maeneo mengi huku Umoja wa Mataifa ukilaani ukandamizaji unaoendelea na kuonya kwamba hali ya haki za binadamu bado ni mbaya.
Msemaji wa jeshi, Zaw Min Tun, amekiri kuwa kuna wakosoaji wa kimataifa lakini ameahidi kuwa uchaguzi huu utaleta utulivu wa kisiasa na mustakabali bora kwa taifa.
CHANZO: Reuters, 28 Desemba 2025




