Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile katikati waliokaa,akiwa katika picha ya pamoja na askari wapya na Wahifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini baada ya kufungua mafunzo yaliyohusu utawala bora,kujikinga na magonjwa yanayoambukiza na yasioambukiza pamoja na ukimwi mafunzo yaliyofanyika ukumbi wa Chandamali Resort mjini Songea,kushoto kwake Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini Manyisye Mpokigwa.
Na Mwandishi maalum,Songea
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini,umeendesha mafunzo kwa wahifadhi wapya 70 kutoka mikoa mitatu ya Lindi,Mtwara na Ruvuma kuhusu utawala bora,kujikinga na magonjwa yasioambukiza,ukimwi na kuwajengea uwezo katika kusimamia rasilimali za misitu na uchumi unaotokana na mazao ya misitu.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Jeshi la Wananchi Tanzania wa Chandamali Resort yalifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile, ambapo ameipongeza TFS kwa kuwapa askari wapya mafunzo ambayo yatawasaidia kusimamia vema rasilimali za misitu kwa ajili ya kuleta matokeo chanya hasa ikizingatia kuwa,sekta ya misitu ndiyo sekta mama kutokana na umuhimu wake.
“Unapotaja utalii na kilimo hautoacha misitu kwa ajili ya chakula na mazingira,mtalii anapokwenda kufanya utalii lazima apite kwenye misitu,mtu anapotaka kufuga mifugo ni lazima atahitaji nyasi,ukitaja kilimo nacho utahitaji misitu ambayo inasaidia sana kuleta mvua,kwa hiyo sekta yenu ina uhitaji mkubwa kwa maisha ya kila siku kwa binadamu”alisema Ndile
Aidha,amewataka watumishi wapya kwenda kuhakikisha kukomesha uharibifu wa mazingira kwa kukata miti au kuchoma moto misitu kwa ajili ya shughuli za kibinadamu hususani kilimo na ufugaji huku akiwasisitiza suala la kuwa waadilifu na kuepuka vitendo vya kuruhusu uvunaji haramu wa misitu.
Ndile,ameitaka TFS ianze kujikita zaidi kwenye kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira ambayo ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai wengine.
Alisema,Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na miti mingi na baadhi ya wananchi wamekuwa wakipanda miti kwa ajili ya biashara,hata hivyo bado kuna uelewa mdogo kuhusu namna ya kuendesha kilimo cha miti na biashara ya mbao.
Ndile,amewakumbusha watumishi hao suala la utii na uaminifu sehemu ya kazi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Serikali ikiwemo kuomba na kupokea rushwa kwa watu wanaotaka kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi kama vile wafugaji.
“Serikalini tuna mambo makubwa mawili ambayo ni utii na uaminifu,ukikosa utii haufai kuwa mtumishi wa umma,nyinyi ni zaidi ya watumishi wa umma na mtumishi mtiifu na mwaminifu,hawezi kuchukua rushwa ”alisema Ndile.
“Nendeni mkasimamie sheria na taratibu zilizowekwa badala ya kutanguliza maslahi binafsi,nyinyi mna mchango mkubwa katika kulinda rasilimali zetu,akija mtu akikupa hata Sh.milioni 10 ili aingize mifugo kwenye misitu kataeni kwani hilo ni kosa kubwa kisheria na katika utumishi wa umma”alisema Ndile.
Kwa upande wake Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini Manyise Mpokigwa alisema,mafunzo haya ni muhimu kwani yamewaongezea wahifadhi na askari wapya uwezo katika kutekeleza majukumu yao kwani watakwenda kufanya kazi kwa weledi kwa kushirikiana na jamii iliyopo kwenye maeneo yao.
Pia alisema,kwenye mafunzo hayo watumishi wamekumbushwa suala la kujikinga na magonjwa yanayoambukiza na yasioambukiza ikiwemo ukimwi ili kuhakikisha TFS inakuwa na watumishi wenye afya njema wanapokuwa wanatekeleza majukumu ya Serikali.
“katika mafunzo yetu ya leo,watumishi wa TFS wameelekezwa namna ya kutunza afya zao na uelewa ili waweze kutumikia taasisi na Serikali kwa ujumla wakiwa na afya njema,ukiangalia kazi zetu mtumishi anatakiwa kuwa na afya njema na nguvu ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo”alisema Mpokigwa.
Alisema,watumishi hao wamekumbushwa suala la maadili kwenye utumishi wa umma kwa kuwa waaminifu kwa Serikali na Taasisi na kufuata sheria na taratibu ili waweze kuwatumikia wananchi ambao ni wadau wakubwa wa sekta mama ya misitu.
Mpokigwa,amewataka watumishi hao kwenda kutekeleza kazi zao kwa kufuata misingi ya utumishi wa umma na kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza kuharibu taswira ya taasisi pale wanapotekeleza wajibu na majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake mtumishi wa TFS kutoka Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Eunike Lugungu,ameishukuru Serikali kwa kuwezesha kupata ajira na kuhaidi kwenda kufanya kazi kwa misingi ya haki,sheria na weledi ili kuongeza tija iliyokusudiwa na Serikali ya awamu ya sita katika usimamizi wa sekta ya misitu.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile,akifungua mafunzo kwa askari wapya wa Wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chandamali Resort mjini Songea,kushoto Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini Manyisye Mpokigwa.
Kamanda wa wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS) Kanda ya Kusini Kamishina Msaidizi Mwandamizi Manyise Mpokigwa,akizungumza na askari wapya wa TFS kwenye mafunzo ya kuwajengea uelewa katika utendaji wa majukumu yao,kujikinga na magonjwa yanayoambukiza na yasioambukiza na utawala bora yaliyofanyika katika ukumbi wa Chandamali Resort mjini Songea,katikati Mkuu wa Wlaya ya Songea Kapenjama Ndile.
Baadhi ya wahifadhi kutoka Wakala wa Huduma za misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini,wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile wakati wa mafunzo maalum kwa askari wapya wa TFS yaliyofanyika katika ukumbi wa Chandamali Resort mjini Songea.




