Arusha. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, kwa kushirikiana na Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi ambaye pia ni Makamu na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Bw. Amon Manyama, wameongoza Mkutano wa nne wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Kujenga Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu dhidi ya Matishio ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
Mkutano huo umefanyika leo Desemba 17, 2025, katika Ukumbi wa Kituo cha Utalii cha Ngorongoro, jijini Arusha, ukiwaleta pamoja wadau wa uhifadhi na utalii kujadili utekelezaji, mafanikio na mwelekeo wa mradi huo katika Hifadhi za Misitu ya Mazingira Asilia nchini.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), UNDP, Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ikolojia ya misitu na kulinda bioanuwai dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Abbasi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa taasisi na wadau katika kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa ufanisi, huku akitaja uhifadhi wa misitu kuwa nguzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustawi wa jamii zinazozunguka hifadhi hizo.
Kwa upande wake, Bw. Manyama alisema UNDP itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kulinda rasilimali za asili, akibainisha kuwa mafanikio ya mradi yanategemea uwajibikaji, usimamizi thabiti na ushirikishwaji wa jamii.
Mkutano huo ulitathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, changamoto zilizopo na kutoa mwelekeo wa utekelezaji kwa kipindi kijacho, ili kuhakikisha misitu ya asili inalindwa na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Awali Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Zainabu Bungwa ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali TFS akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi alieleza utayari wa TFS kutekeleza maelekezo ya Kamati kwa wakati na kwa Usahihi. Aidha aliendelea kuhimiza ushirikiano wa wadau hawa ili kuendelea kupata ufadhili kutoka Mfuko wa Mazingira (GEF).




