Na Mwandishi wetu, Simanjiro
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, amewataka vijana wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kuchangamkia fursa ya mikopo ya shilingi bilioni 200 zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Ole Millya ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Simanjiro amewataka vijana kuhakikisha wanaomba mikopo katika fedha hizo ambazo zinatolewa katika siku 100 za mwanzo wa utawala wa awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye kata ya Komolo wilayani Simanjiro, akiwahamasisha vijana kuchangamkia fursa hizo ili wajinufaishe kiuchumi.
“Kuna shilingi bilioni 200 zinatolewa katika siku 100 za mwanzo wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan hivyo vijana wenzangu wa Simanjiro tuchangamkie fursa hiyo,” amesema Ole Millya.
Amewataka vijana wa Simanjiro kuandika miradi na kuomba mkopo kupitia fedha hizo kwani Tanzania nzima wanapaswa kupatiwa.
“Vijana wa Simanjiro changamkieni fursa hizo kwani hakuna mtu ataweza kukupikia na kukulisha tunamshukuru Rais Samia kwa kutukumbuka vijana,” amesema Ole Millya.
Amesema hivi sasa kila Wizara inajitahidi kutimiza wajibu wake hivyo na vijana wa Simanjiro nao wahakikishe wanapambania fursa hiyo ya mikopo.
“Tunamshukuru Mungu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuniona mimi kijana wa jamii ya kifugaji wa Simanjiro, ambaye nimetoka kwenye familia ya kawaida kuwa msaidizi wake na kuwa Naibu Waziri,” amesema Ole Millya.



