NA DENIS MLOWE, IRINGA
DIWANI wa Viti Maalum Kanda ya Kihesa, Bi. Sara Ponela, kwa kushirikiana na Diwani wa kata ya Kihesa katika Halmashauri ya Manispaa Iringa Hosea Kabelege wamewataka wananchi wa Kihesa kuunga mkono na kushiriki kikamilifu katika mradi wa ujenzi wa soko la Kihesa unaolenga kukuza uchumi wa wananchi na kuboresha mazingira ya biashara.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi za kata Kihesa, Diwani Ponela alisema mradi huo ni wa muhimu kwa maendeleo ya wananchi, kwani utatoa ajira wakati wa ujenzi na pia fursa za kudumu za biashara baada ya kukamilika.
“Ujenzi wa soko hili ni fursa kwa akina mama, vijana na wajasiriamali kuongeza kipato na kupata maeneo bora ya kufanyia biashara,” alisema Diwani Ponela.
Kwa upande wake Mkandarasi mradi huo
Injinia Mbulinyingi Nkumulwa kutoka kampuni ya Dimetoclasa Realhope Limited ya jijini Dar es Salaam alisema mradi huo utatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji na kuwahakikishia kwamba kipaumbele katika ajira utaanza na wakazi wa kata hiyo na mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Alisema kuwa wameingia mkataba na serikali kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko hilo na barabara zinazounganisha kata ya Mkimbizi na Mtwivila vyote vikiwa na thamani ya bilioni 20.
“Mazingira ya mradi yatalindwa na miundombinu itakayojengwa itazingatia mahitaji ya makundi yote, ikiwemo watu wenye ulemavu,” alisema mhandisi huyo.
Naye Diwani wa kata ya Kihesa Hosea Kabelege aliongeza kuwa kukamilika kwa soko hilo kutachangia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Mjini, yatakayorejeshwa kwa wananchi kupitia huduma za jamii kama elimu, afya na miundombinu.
Aidha alisema kuwa kipaumbele cha kwanza mara baada ya kukamilika kwa mradi huo ni wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara zao kabla ya kuvunjwa kwa soko hilo.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walieleza matumaini yao kuwa ujenzi wa soko hilo utaboresha biashara zao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Kanda ya Kihesa.
Mradi wa ujenzi wa soko la Kihesa unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya kukamilika kwa taratibu za awali ambapo utachukua miezi 15 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2026.




