Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Uwakilishi, iliyofunguliwa na waliokuwa wagombea wa ACT-Wazalendo, imetajwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu Zanzibar.
Kesi hiyo ilitajwa mbele ya Naibu Mrajisi Faraji Shomar Juma katika Mahakama Kuu iliyopo Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, na imeahirishwa hadi tarehe 18 Desemba 2025, ambapo itatajwa tena kwa mara ya pili.
Awali, wakili wa upande wa walalamikaji, unaoongozwa na Wakili Omar Said Shaaban, aliomba Mahakama itoe hati ya majibu ya upande wa Serikali ili walalamikaji waweze kuyapitia kabla ya hatua zaidi za usikilizwaji.
Kwa upande wa Serikali, Jopo la Mawakili wa Serikali likiongozwa na Mbarouk Suleiman Othman kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, lilikubali kutoa majibu hayo, lakini likatoa angalizo kuwa majibu hayo yasitumike kupitia pingamizi ambazo tayari wameziwasilisha katika utetezi wao.
“Mheshimiwa Naibu Mrajisi, sisi hatuna tatizo na kupewa majibu, lakini wasije wakayatumia kupitia pingamizi tulizowasilisha,” alisema Wakili Mbarouk.




