Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo Ahmed Abbas kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika ukumbi wa Halmashauri mjini Namtumbo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo Philemon Magesa akitoa taarifa ya utekelezaji kwenye kikao cha Baraza la madiwani.

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ngollo Malenya,akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Namtumbo,kulia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas na kushoto Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas,akizungumza na watumishi na madiwani kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo,kulia Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo France Pilly.
…………
Na Mwandishi Wetu, Namtumbo
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas,amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Namtumbo,kuepuka kuzalisha migogoro na watumishi badala yake wafanye kazi kwa ushirikiano na uwazi ili kuleta maendeleo ya kweli kwa manufaa ya wananchi wa Halmashauri hiyo na Mkoa wa ujumla.
Abbas,amesema hayo jana wakati akizungumza na madiwani,watumishi na baadhi ya wananchi kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo mjini Namtumbo.
Alisema,migogoro na kutoelewana kati ya watendaji na madiwani ni miongoni mwa vitu vinavyosababisha kukwama kwa shughuli mbalimbali za maendeleo katika eneo lolote,hivyo asingependa kuona maendeleo katika Halmashauri ya Namtumbo yanakwamisha kwa sababu sizokuwa na msingi au maslahi ya watu fulani.
Alisema,uongozi bora uanza pale madiwani wanapoweka maslahi ya wananchi mbele badala ya maslahi yao na madiwani ni Daraja kati ya ndoto za wananchi na utendaji wa kimaendeleo katika Halmashauri yoyote na baraza imara la madiwani utengeneza Halmashauri imara na bora.
Aidha alisema,uadilifu wa madiwani unaweza kubadilisha maisha ya watu wengi kwa uamuzi wenye busara na nguvu ya baraza ipo kwenye dhamira ya dhati iliyowasukuma kuomba uongozi kutoka kwenye kata zao na kuhakikisha kila hoja inayoletwa kwenye vikao vya baraza zitumike kuleta matokeo chanya kwenye Halmashauri yao.
Alisema,madiwani wakiwa na umoja wananchi hupata matumaini na wakifanya mambo kwa haki jamii inaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo tena kwa haraka.
Abbas,amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Philemon Magesa kwa kazi nzuri aliyofanya kuongeza mapato ya ndani kutoka Sh.bilioni 2 mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Sh.bilioni 4 mwaka 2024/2025.
Abbas, amewataka madiwani kwenda kufanya kazi kama timu kwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kutosita kuwachukulia hatua watumishi wote watakaosika katika kushindwa kusimamia na upotevu wa mapato ya ndani na Halmashauri kuhakikisha inafanya matumizi sahihi ya fedha kulingana na mapato yanayokusanywa.
“nendeni mkasimamie miradi inayotekelezwa katika kata zenu na akikisheni inalingana na gharama halisi ya fedha zinazoletwa, pia mkamilishe miradi yote viporo badala ya kuanzisha miradi mipya ili kujenga imani kwa wananchi”alisema Abbas.
Abbasa,amewasisitiza madiwani kuhakikisha wanashiriki moja kwa moja kwenye ukaguzi wa miradi,kusikiliza mahitaji ya wananchi wa maeneo husika na kuepuka kupeleka miradi ambayo wananchi hawahitaji.
Amewakumbusha madiwani na viongozi wengine katika jamii,kuendelea kuhimiza suala la amani na utulivu, kwa sababu wanayo nafasi kubwa ya kusikilizwa na wananchi wao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho,amewaasa madiwani kwenda kudumisha mahusiano kwa wananchi na watendaji wa Serikali wakiwemo watendaji wa vijiji na kata kwenye maeneo yao ili kwa pamoja waweze kusukuma maendeleo.
“Baadhi ya madiwani waliopita kazi yao ilikuwa blaa blaa tu badala ya kufanya kazi walikuwa wanashinda mjini na hadi walipewa majina ya madiwani wa mjini,hawa watendaji ni binadamu sio malaika,mkavumiliane na kushirikiana ili kwa pamoja muweze kuwaletea wananchi maendeleo”alisema Mwisho.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya,amewaomba madiwani wapya kwa kushirikiana na wakuu wa idara kuhakikisha wanasikiliza kero za wananchi na kuzitatua wanazoona ziko chini ya uwezo wao.
Amewataka madiwani hao,kuwa watumishi kwa wananchi na kwenda kupunguza malalamiko na manung’iniko badala ya kuwa mabosi ili kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika majukumu ya kuwatumikia Watanzania.
“Leo tumeapa lakini tusiende kuwa mabosi Hapana,sisi ni watumishi wa wananchi ambao wametupa dhamana hiyo,tusiweke vizuizi kwao tutengeneze mazingira mazuri ili wananchi waweze kutufikia,tuwe na mahusiano mazuri kati ya wananchi na Serikali ili kazi za Rais Samia Suluhu Hassan ziweze kwenda vizuri”alisema Dc Ngollo.
Katika kikao hicho madiwani walimchagua diwani wa kata ya Msisima France Kamenya kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kwa kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa Kamenya amehaidi kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu,kuunganisha watumishi,watendaji na wananchi ili kwa pamoja waweze kuharakisha maendeleo na uchumi wa Wilaya ya Namtumbo.




