
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda akizungumza na wanachama wa TRA SACCOS LTD wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 20 wa Mwaka wa TRA SACCOS LTD iliyofanyika leo Desemba 6, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya TRA SACCOS LTD, CPA Mbogo Kerenge akizungumza na wanachama wa TRA SACCOS LTD wakati Mkutano Mkuu wa 20 wa Mwaka wa TRA SACCOS LTD iliyofanyika leo Desemba 6, 2025 jijini Dar es Salaam.

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amewataka wanachama wa TRA SACCOS LTD kuongeza jitihada katika kuhamasisha wananchi na watumishi kujiunga na chama hicho, pamoja na kuendeleza ubunifu utakaowezesha ushindani katika sekta ya fedha.
Amesema kuwa hatua hizo zitawasaidia wanachama kupata uhuru wa kifedha, kufanya kazi kwa ufanisi, na kuepuka vishawishi vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza leo, Desemba 6, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Mwaka wa TRA SACCOS LTD, Bw. Mwenda amesema kuwa lengo la SACCOS ni kuchochea ukuaji wa uchumi wa wanachama na Watanzania kwa ujumla, na hivyo ni muhimu kwa wanachama kuwa mabalozi wa uchumi wa Taifa.
Bw. Mwenda ameipongeza TRA SACCOS LTD kwa mafanikio makubwa waliyoyapata, huku akisisitiza umuhimu wa uadilifu katika utendaji wa kazi.
Ameeleza pia kuwa SACCOS ni njia sahihi ya kuwawezesha watumishi kumiliki mali kwa njia halali.
“Kumiliki mali ni haki ya kikatiba, lakini mali hizo lazima zipatikane kwa njia halali. SACCOS inatoa fursa ya kukopesha watumishi na kuwasaidia kutimiza haki yao ya kikatiba. Mimi nitakuwa balozi wa TRA SACCOS ili kuhakikisha inakuwa chama bora na kinara katika huduma za akiba na mikopo Tanzania,” amesema Bw. Mwenda.
Aidha, ameongeza kuwa mtumishi wa TRA ili aweze kufanya kazi kwa ufanisi anahitaji kuwa na uhuru wa kifedha, na hivyo TRA SACCOS itatumika kuwawezesha watumishi kufikia malengo yao.
Amewataka wanachama kuendelea kuhamasisha ulipaji sahihi wa kodi, pamoja na kuwashauri wanaochukua mikopo kuitumia kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo yenye tija.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA SACCOS LTD, CPA Mbogo Kerenge, amesema kuwa chama hicho ni miongoni mwa vyama vitatu vyenye mitaji mikubwa zaidi nchini.
Amebainisha kuwa wameanzisha pia huduma za kibenki ndani ya SACCOS, ikiwemo kupokea fedha za wanachama waliostaafu na kuwapa fursa ya kukopa hadi milioni 50 kwa riba ndogo, ili kuwasaidia katika maisha yao baada ya kustaafu.




