Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein akizungumza leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwagoha, akizungumza leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City.
Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wakiwa katika Mahafali ya 24.

Wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe wakiwa katika maandamano
………….
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, amewataka wahitimu wa chuo hicho kuendelea kujielimisha, kuchangamkia fursa zilizopo na kutumia maarifa waliyoyapata kutatua changamoto za kijamii.
Akizungumza leo Desemba 4, 2025 jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Dkt. Shein amesema kuwa ni muhimu wahitimu kufuatilia fursa kupitia mbinu mbalimbali kwa kutumia elimu, ujuzi na maarifa yao.
“Nendeni mkakabiliane na changamoto za maisha mapya kwa uweledi, busara na nidhamu. Fanyeni kazi kwa bidii bila kukata tamaa,” amesema Dkt. Shein.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwagoha, amesema chuo kimeendelea kuboresha miundombinu ya kujisomea, kujifunzia na utendaji kazi, ikiwemo mifumo ya TEHAMA pamoja na ujenzi wa viwanja vya michezo eneo la Tegeta.
Ameeleza kuwa chuo kimekuwa kikiandaa mafunzo, mikutano, makongamano na mihadhara mbalimbali kwa wanafunzi, hususan vijana wa kizazi cha sasa (Gen Z), kwa kushirikiana na makampuni na wataalamu mbalimbali ili kuwaimarisha kitaaluma, kijamii na kuwajengea maadili, uzalendo na uwajibikaji katika kulinda rasilimali na tunu za taifa.
Miongoni mwa mikutano hiyo ni ule wa Makampuni ya Norway (NHO) ulioratibiwa na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania, pamoja na mafunzo kuhusu kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuhamasisha uanzishwaji wa vilabu vya kupambana na rushwa.
Prof. Mwagoha ameeleza kuwa katika mwaka wa masomo 2024/2025, chini ya uongozi wa Baraza la Chuo na kwa ushirikiano wa Menejimenti, Wafanyakazi na Wanafunzi, chuo kimeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kama yalivyoainishwa katika Hati Idhini ya mwaka 2007, Mpango Mkakati wa Tano, Sheria ya Vyuo Vikuu ya 2025 pamoja na sera, kanuni na maelekezo ya Serikali.
Kwa sasa, Ndaki ya Dar es Salaam ina jumla ya wanafunzi 1,793, ambapo 1,027 wa Shahada za Umahiri na 766 wa Shahada ya Awali.
Kati yao, wanaume ni 854 (asilimia 47.6) na wanawake 939 (asilimia 52.4), ikionyesha mwitikio mkubwa wa wanafunzi wa kike kujiendeleza kielimu.
Katika mahafali haya, jumla ya wanafunzi 752 wanatunukiwa stahiki zao katika ngazi tofauti za kitaaluma. Kati yao, 560 wanahitimu Shahada za Umahiri—wanaume 251 (asilimia 44.8) na wanawake 309 (asilimia 55.18). Wengine 192 wanahitimu Shahada ya Kwanza/ Awali, ambapo 82 (asilimia 43) ni wanawake na 110 (asilimia 57) ni wanaume.
“Nawapongeza kwa juhudi, uvumilivu na nidhamu mliyokuwa nayo hadi kufanikisha masomo yenu. Mafanikio haya si mwisho wa safari, bali mwanzo wa hatua mpya za maisha. Elimu mliyopata ni hazina na silaha ya kubadilisha maisha yenu na jamii. Ni wajibu wenu kutumia maarifa haya kwa uadilifu, ubunifu na ari ya kuleta maendeleo,” amesema Prof. Mwagoha.
Kwa upande wao, wahitimu wameahidi kuwa mabalozi wazuri wa Chuo Kikuu Mzumbe na kutumia ipasavyo maarifa waliyoyapata.



