

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Akizungumza na Menejimenti ya Watumishi Housing Investment (WHI) katika kikao kazi kilichofanyika leo Novemba 27, 2025, katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Arch. Sephania Solomon akitoa taarifa ya utendaji kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete katika Kikao kazi kilichofanyika leo Novemba 27, 2025, katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na wafanyakazi wa WHI
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameitaka Menejimenti ya Watumishi Housing Investment (WHI) kuongeza juhudi katika ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma katika maeneo yenye uhitaji mkubwa, ili kupunguza changamoto za makazi kwa watumishi hao.
Akizungumza na Menejimenti ya WHI katika kikao kazi kilichofanyika leo Novemba 27, 2025, katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, Mhe. Kikwete amesema kuwa wakati umefika wa kutafsiri maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo, kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.
Amesema ni muhimu kubuni mbinu mbadala za kupata mapato kwa ajili ya kutekeleza miradi ya nyumba, badala ya kutegemea bajeti ya Serikali.
“Tunaweza kufanya makubaliano na halmashauri ili kujenga nyumba za watumishi kwa urahisi, jambo litakalosaidia kufikia malengo na kuongeza tija kwa Taifa,” amesema Mhe. Kikwete.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujenga nyumba kulingana na thamani halisi ya soko kwa kutumia teknolojia isiyoongeza gharama, ili kuhakikisha miradi inabaki kuwa nafuu na bora.
“Nimetembelea mikoa mbalimbali na kuona kazi nzuri inayofanywa na WHI. Naomba muendelee kujenga nyumba zenye ubora na ufanisi,” ameongeza.
Pia amehimiza kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya WHI na huduma zake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Arch. Sephania Solomon, amemshukuru Waziri Kikwete kwa kutembelea ofisi hizo na ameahidi kutekeleza maagizo yote kwa lengo la kuongeza tija na kufanikisha malengo ya taasisi.
Ameeleza kuwa WHI inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma, na kwamba miradi hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam na Dodoma.



