Na. Joyce Ndunguru, Morogoro.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt Ashatu Kijaji (Mb) amewataka watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuzingatia utu, sheria na haki katika utekelezaji wa majukumu ya ulinzi wa rasilimali za Taifa.
“_Sisi watumishi wa umma tunapaswa kutoa huduma kwa wananchi kwa haraka na kwa viwango huku tukizingatia haki, sheria na utu wa wananchi tunaowahudumia_” amesema Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji ameyasema hayo, leo Novemba 24,2025, katika ziara yake ya kwanza ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA zilizopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kujifunza, kujionea jinsi shughuli za uhifadhi na utalii za TAWA zinavyofanyika na kujitambulisha kwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Pia, Dkt. Kijaji amesisitiza kuendelea kuimarishwa kwa ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori katika maeneo ya hifadhi kwa kuongeza ufanisi katika doria, ujenzi wa vituo vya askari na matumizi ya teknolojia kama ndege nyuki (drones) na visukuma mawimbi ( GPS Collars).
Sambamba na hayo, Mhe.Dkt. Kijaji amezindua vitendea kazi ambavyo ni magari (4) ya shughuli za doria, pikipiki (33) kwa ajili ya shughuli ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na pikipiki ya miguu mitatu (Bajaji) iliyokabidhiwa kwa Askari wa Uhifadhi, Elihuruma Rashid aliyepata changamoto za kiafya akiwa katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande (Mb) amesema kwamba, vitendea kazi hivi vilivyozinduliwa leo ni jitihada zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya wanyamapori.
Kwa upande wake, akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema kuwa Bodi itahakikisha kuwa maelekezo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa ubunifu na weledi wa hali ya juu.
Aidha, Mej. Jen (Mstaafu) Semfuko ameongeza kuwa TAWA itaendelea kuhakikisha kuwa jamii zinazopakana na hifadhi zinafaidika kutokana na rasilimali zilizopo katika maeneo hayo.
Awali, akimkaribisha Mhe. Dkt. Kijaji, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yussuf Kabange amesema TAWA ina jukumu kubwa la kuhakikisha rasilimali za wanyamapori zinalindwa katika maeneo yanayoisimamia yakiwemo Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu hivyo kuongezeka kwa vitendea kazi hivi kutachagiza ufanisi wa shughuli za doria katika maeneo mbalimbali.
Kadhalika, Kamishna Kabange ameongeza kuwa jitihada mbalimbali zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya utalii zimeweza kuongeza idadi ya watalii kutoka katika mataifa ambayo awali yalikuwa hayana idadi kubwa ya wageni.
“_Jitihada hizi za Mhe. Rais zimewezesha TAWA kupata kampuni ya mwekezaji wa kwanza kutoka Nchini China aliyewekeza katika shughuli za uwindaji wa kitalii,_” amesema Kamishna Kabange.
Katika ziara hii, Mhe. Kijaji aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, Katibu Mkuu wa Wizara ya Malisili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi na Viongozi wengine wa Wizara ya Malisili na Utalii.




