Na, WAF- Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, leo Novemba 24, 2025 ametoa waraka mahsusi unaoanzisha utekelezaji wa mkakati wa kuendeleza viwanda vya dawa na bidhaa za afya nchini, hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya kwa uhakika ndani ya Tanzania.
Akizungumza mbele ya wataalam wa sekta ya afya katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amesema mpango huo unatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025–2030 na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ukiwa na malengo ya kujenga uwezo wa kitaifa wa uzalishaji wa bidhaa za afya.
Aidha, amesema Serikali inataka kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa sekta binafsi katika viwanda vya dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyingine za afya pamoja na kuiongezea Bohari ya Dawa (MSD) uwezo wa kununua, kuzalisha na kusambaza bidhaa hizo kwa ufanisi.
Katika maelekezo yake, Waziri Mchengerwa amemtaka Katibu Mkuu Wizara ya Afya kuunda kikosi kazi maalum ndani ya siku saba ili kuratibu na kuharakisha utekelezaji wa mkakati huo.
Aidha, ameagiza kuandaliwa orodha kamili ya wawekezaji wote waliowahi kuonyesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya dawa tangu mwaka 2015 ikiwa na hatua walizofikia, vikwazo, mahitaji ya rasilimali, uwezo wa kifedha pamoja na sababu za ucheleweshaji na kuiwasilisha kwake ndani ya siku 15.
Pia, Mhe. Mchengerwa ameelekeza kufanyika mkutano wa pamoja na wawekezaji wote ndani ya siku 30 ili kujadili changamoto, kuweka maazimio ya utekelezaji na kufungua milango kwa wawekezaji wapya.
Kwa lengo la kuongeza mvuto wa uwekezaji, Waziri ameagiza Wizara ndani ya siku 21 kutangaza rasmi fursa za uwekezaji katika bidhaa za afya kupitia tovuti za Serikali, taasisi za uwekezaji na maeneo maalum ya kiuchumi (TISEZA).
Aidha, Waziri Mchengerwa ameelekeza kuanzishwa kwa kitengo maalumu cha uwekezaji ndani ya Wizara kitakachokuwa chini ya ofisi ya Waziri, chenye jukumu la kuratibu wawekezaji, kutoa taarifa kwa wakati, kufuatilia maamuzi ya kikosi kazi na kusimamia taratibu za vibali.
Waziri Mchengerwa amehimiza watalaam wa sekta ya afya kuongeza uwajibikaji, ubunifu na kasi ya utekelezaji ili kuhakikisha waraka huo unaleta matokeo chanya kwa taifa, ikiwemo kupunguza gharama za huduma kwa wananchi na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya nchini.




