Na Meleka Kulwa -Dodoma
Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) leo Novemba 20, 2025 kimefanya kongamano maalum katika tawi lake la Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha machapisho ya tafiti za wanafunzi wa Shahada ya Uzamili, ikiwa ni sehemu muhimu ya masharti ya kuhitimu kwa ngazi hiyo. Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa chuo, watendaji, wanafunzi na wadau mbalimbali wa elimu.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Prof. Eliamani Sedoyeka, alisema AIA ikiwa ni chuo cha Serikali chenye makao makuu Arusha na matawi sita ya Arusha, Dar es Salaam, Manyara, Songea na Geita, kimeendelea kupanua wigo wa utoaji elimu kwa viwango vya kimataifa.
“Chuo chetu kinatoa kozi katika maeneo ya uhasibu, fedha, TEHAMA, biashara na fani mbalimbali za kijamii katika ngazi za cheti, diploma, shahada na uzamili. Kwa wanafunzi wa masters, kufanya utafiti na kuusambaza rasmi kupitia machapisho au wasilisho la kitaaluma ni mojawapo ya vigezo muhimu vya kuhitimu,” alisema Prof. Sedoyeka.
Profesa huyo aliongeza kuwa kwa mwaka huu pekee, chuo kinatarajia kutunuku zaidi ya wahitimu 2,500 kutoka matawi yake yote, hatua inayoonyesha kasi ya ukuaji wa chuo hicho nchini.
Akitaja mwelekeo wa chuo katika utoaji wa elimu, Prof. Sedoyeka alisema programu za uzamili hutolewa kwa njia mbili ya darasani na masafa, hali inayowawezesha Watanzania wote waliopo ndani na nje ya nchi kupata elimu kwa urahisi kupitia vipindi vya moja kwa moja au vilivyorekodiwa.
IAA ina vitivo vitano vya TEHAMA, Biashara, Uhasibu na Fedha, Humanities pamoja na Usalama na Ulinzi. Tafiti za wanafunzi hutokana na changamoto halisi zinazowakabili Watanzania, kwa lengo la kuzitafutia majawabu ya kitaaluma na kuzisaidia jamii.
“Tunawaambia wahitimu kwamba kumaliza masomo si mwisho wa kujifunza. Tafiti zao zina mchango mkubwa kwa Taifa, na kama chuo tutazifanyia tafsiri ya Kiswahili ili kila Mtanzania aweze kuzisoma na kuzitumia,”alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Uhasibu wa AIA, Dkt. Elizius Kalugendo, aliyewasilisha mada kuhusu maendeleo endelevu, alisema dunia ya leo inahitaji wataalamu wanaojua kutunza mazingira na kutoa taarifa sahihi kuhusu mwenendo wake.
“Jukumu hili limekabidhiwa wahasibu na wataalamu wa fedha. Wanapaswa kuonyesha namna tunavyotumia rasilimali za mazingira kwa ustawi wa vizazi vijavyo,” alisema.
Alitoa wito kwa wananchi kuendeleza nidhamu ya utunzaji mazingira na matumizi sahihi ya rasilimali za nchi.
Meneja wa IAA tawi la Dodoma, Dkt. Grace Temba, alisema tawi hilo lilipoanzishwa mwaka 2021 lilikuwa na wanafunzi 51 pekee wa uzamili, lakini leo limekua na kufikia wanafunzi 1,500 watakaohitimu mwishoni mwa mwezi Desemba.
“Leo tunashuhudia hatua muhimu ya wanafunzi wetu. Takribani wanafunzi 600 wapo hapa Dodoma wakitoa matokeo ya tafiti zao, na zaidi ya wanafunzi 700 wa mtandaoni nao wanawasilisha kwa njia ya online,” alifafanua Dkt. Temba.
Alisema machapisho ya tafiti hizo hayatabaki kwenye makabrasha pekee, bali chuo kimepanga kuanza kuyatoa katika majarida mbalimbali na kwenye majukwaa ya kidijitali ndani ya muda mfupi ujao.
Dkt. Temba alibainisha kuwa moja ya malengo ya kongamano hilo ni kuzitumia tafiti za wanafunzi kuinua biashara ndogondogo jijini Dodoma kwa kuwapa ufahamu wa kitaalam na suluhisho la changamoto wanazokumbana nazo.
Wanafunzi waliofanya uwasilishaji, akiwemo Issa Nyatuka na Alfredina Mulokozi, walieleza namna tafiti zao zinavyoweza kutatua changamoto katika jamii na kutoa mwanga kwa watunga sera, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.
Kwa ujumla, kongamano hilo limetajwa kuwa mwanzo wa zama mpya za utafiti ndani ya chuo, huku likiahidi kuendeleza mchakato wa kuchochea maarifa, ubunifu na maendeleo ya jamii kupitia tafiti bunifu zenye tija kwa Taifa.




