Na mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mwalimu Fakii Raphael Lulandala amemfuta machozi mjane Sion Mathayo mkazi wa kitongoji cha Mkumbi mji mdogo wa Orkesumet kwa kufanikisha kulipa Sh11 milioni ya deni la nyumba yake iliyowekwa rehani na mume wake dereva bodaboda Mohamed Ally (Mang’ati) aliyeuawa hivi karibuni.
Dereva bodaboda huyo Mohamed Ally (Mang’ati) ambaye aliuza nyumba yake ili kufidia deni alilokuwa anadaiwa, aliuawa kwa kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na watu wawili alipokuwa na pikipiki yake Oktoba mwaka 2025 kisha akafariki dunia akipatiwa matibabu.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Lulandala akizungumza wakati akimkabidhi mjane huyo hati ya nyumba hiyo amesema wadau mbalimbali wamechanga fedha na kulipa deni hilo ili aendelee kuishi na mtoto wake kwenye nyumba hiyo, baada ya mumewe kuuawa.
“Mume wake kabla hajafariki alipata masaibu na kuuza rehani nyumba yao kwa Sh11 milioni ili alipe deni analodaiwa kisha akachomwa moto na kufariki dunia, nikazungumza na wadau ili tulipe fedha hizo na mjane aendelee kuishi hapo,” amesema Lulandala.
Amesema watu mbalimbali wamechangia fedha hizo hadi kupatikana kwake ikiwemo ofisi yake, Mbunge wa Simanjiro na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Ole Millya na wadau wengine wa maendeleo.
“Nawapongeza wote waliochangia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha mjane anaendelea kuishi kwenye nyumba yao kwani deni ndilo limesababisha yote kutokea,” amesema mwalimu Lulandala.
Kwa upande wake mjane huyo Sion Mathayo amemshukuru mkuu wa wilaya hiyo kwa kufanikisha kulipa deni na kupata nyumba hiyo ambayo mume wake aliiuza ili kufidia deni alilokuwa anadaiwa kabla hajauawa.
“Namshukuru Mungu kwa tukio hili la DC wetu Mhe Lulandala kusimamia kupatikana kwa fedha hizo na sisi kuendelea kuishi katika nyumba yetu ambayo marehemu mume wangu aliiuza ili afidie deni alilokuwa anadaiwa,” amesema Sion.
Amesema japokuwa hivi sasa amempoteza mume wake aliyeuawa ila amefarijika yeye na mtoto wake wataendelea kuishi katika nyumba yao.
Mwenyekiti wa madereva waendesha bodaboda wa mji mdogo wa Orkesumet, Joshua Lemomo Kishumuu amesema kitendo cha mkuu wa wilaya kurejesha nyumba kwa mjane huyo ni cha kupongezwa mno.
“Tunamshukuru DC wetu mwalimu Lulandala kwa kusimama kidete kwani nyumba ilishauzwa na mjane angeteseka ila hivi sasa ataendelea kuishi hapo tofauti na awali kwani alikata tamaa,” amesema Kishumuu.
Mmoja kati ya wakazi wa Orkesumet, Enot Paul amesema ni jambo jema kwa mjane huyo kuendelea kuishi katika nyumba hiyo kwani angepata mapigo mawili ya kuondokewa na mume na kukosa nyumba.
“Ni tukio zuri la mjane kupata msaada huu kwani mume wake alikuwa dereva bodaboda kisha akauawa na pia akatakiwa kuondoka kwenye nyumba anavyoishi ila sasa amefarijika,” amesema.



