Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo akizungumza kwenye Baraza la Wafanyakazi Jijini Mwanza

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa kwenye mkutano

Picha ya pamoja
……
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katika kuhakikisha Sekta ya madini inakuwa na kuendelea kuwanufaisha watanzania pamoja na kukuza mchango wa sekta katika Pato la Taifa Wizara imejiwekea vipaumbele saba vitakavyo leta tija nchini.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Novemba 20, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo Jijini Mwanza.
Mbibo amevitaja vipaumbele hivyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa,kuendeleza mnyoro wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati, kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo.
“Tutahamasisha uwekezaji na uongezaji thamani madini pia tutaongeza uwekezaji kwenye tafiti za kina za madini,tutaimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya Vito pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara ya madini ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi”, amesema Mbibo
Aidha, ameeleza kuwa kumekuwa na utekelezaji mzuri wa malengo waliyojiwekea katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2025 ambapo mafanikio mbalimbali yamefikiwa ikiwa ni pamoja na makusanyo ya maduhuli yaliyokusanywa na kuwasilishwa hazina kwa kipindi hicho ni shilingi bilioni 430.1, sawa na asilimia 35.85 ya lengo la mwaka wa fedha 2025/26 ikiwa lengo la makusanyo ya mwaka mzima ni shilingi trilioni 1.19.
Mbibo amesisitiza kuwa uwepo wa Baraza la Wafanyakazi katika sehemu za kazi ni matakwa ya kisheria, hivyo amehimiza wawakilishi wote wa baraza hilo kutoa maoni na mapendekezo yao kwa uhuru ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa wizara.
Kwaupande wake Kaimu Afisa Kazi Dodoma, Eunice Mmari amewasihi Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kuwasilisha hoja za wafanyakazi wenzao huku akiwataja wao kuwa muunganiko mkubwa ambapo wanaweza kuhakikisha tija inatimizwa katika wizara ya madini.
“Haki ni wajibu na wajibu ni haki hivyo kupitia nyie mtahakikisha wafanyakazi wengine wanatimizi wajibu katika utendaji wao wa kazi”, amesema Mmari
Naye Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi nchini Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Mara, Hamisi Mwisa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa ameipongeza Wizara ya Madini kwa kufanikisha mkutano huo muhimu, huku akitoa wito kwa watumishi kushiriki kikamilifu kutoa maoni yatakayoboresha masilahi na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Wizara ya Madini.



