Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amewataka wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchini kujipanga vizuri na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 kwa kuweka mikakati inayowezesha huduma endelevu ya majisafi na usafi wa mazingira nchini.
Amesema hivyo wakati akifungua kikao kazi cha Wakurugenzi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira mkoani Morogoro.
Mhandisi Mwajuma amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 20250 inalenga kuwa na taifa lenye uhakika na usalama wa maji kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kudumisha na kuendeleza ekolojia. Pia kuwa na taifa lenye mfumo imara na shirikishi wa usimamizi wa ardhi oevu na rasilimali nyinginezo. Hivyo, hayo yote yanatoa ujumbe kwa watendaji wa Sekta ya Maji kujipanga kwa kuwa wabunifu ili kuhakikisha malengo yanafikiwa.
Amesisitiza kuwa pamoja na kuwa maji ni suala la kijamii pia ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi ambapo mamlaka za majisafi zinajukumu la kuhakikisha maji ya kutosha na yenye viwango sahihi vya ubora yanapatikana.
Ametaja maeneeo mengine ambayo yanatoa kipaumbele na kuwapa jukumu hao ni pamoja na Sera ya Maji ya mwaka 2002 toleo la mwaka 2025 ambayo pamoja na masuala mengine inasisitiza kuwa na gridi ya Taifa ya maji, programu ya kusaidia Sekta ya Maji awamu ya pili ambayo inafikia ukomo na kufanya hitaji la kuwa na programu ya awamu ya tatu, Pia Dira ya Maji ya Afrika ya mwaka 2063 .
Amesisitiza kuwa mahitaji hayo yote yanalenga kuwepo na upatikanaji wa fedha hivyo Mamlaka za maji zijikite kuwa na ubunifu katika kupata rasilimali fedha.
Kikao kazi hicho kinafanyika kwa lengo la kushirikishana njia mbalimbali za utatuzi wa changamoto za utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira ili kufanikisha hitaji la msingi la kufikia utoaji wa huduma hiyo kwa jamii.




