Mhe. Daniel Baran Sillo ni kiongozi makini na mtumishi wa umma mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya fedha, kodi, na uongozi wa kibunge.
Kwa sasa, anahudumu kama Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mkoa wa Manyara.
Elimu
Mhe. Sillo ni msomi aliyejikita katika taaluma ya fedha na usimamizi wa kodi. Ana shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA) katika Fedha, na Post Graduate Diploma in Tax Management, sambamba na Advanced Diploma in Accountancy. Elimu yake imemjengea uwezo mkubwa katika uchambuzi wa masuala ya bajeti, uchumi na usimamizi wa rasilimali za umma.
Uzoefu wa Kazi
Kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa, Mhe. Sillo alitumikia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kipindi cha miaka 20 (2000–2020) akiwa Afisa Mwandamizi, ambapo alijipatia uzoefu mkubwa katika usimamizi wa mapato, ukusanyaji wa kodi, na uwajibikaji wa kifedha.
Safari ya Kisiasa
Mhe. Daniel Sillo alianza safari yake ya kisiasa kwa kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Babati Vijijini mwaka 2015, ambapo hakufanikiwa. Hata hivyo, hakukata tamaa — mwaka 2020, aligombea tena kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda kwa kishindo, akawa Mbunge wa Babati Vijijini katika Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tangu kuingia bungeni, amejipambanua kwa umahiri, nidhamu, na uwezo mkubwa wa kuchambua sera za kiuchumi, jambo lililomfanya kuaminiwa na viongozi wenzake kushika nafasi mbalimbali za juu ndani ya Bunge.
Nafasi alizowahi kushika
- Naibu Waziri – (Machi 2024 hadi Novemba 2025)
- Mwenyekiti wa Bunge – (Aprili 2023 hadi Machi 2024)
- Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti – (Januari 2021 hadi Machi 2024)
- Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge
- Mjumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge
- Mjumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
- Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini – (2020–2025)
- Afisa Mwandamizi wa TRA – (2000–2020)
Uongozi na Uadilifu
Mhe. Sillo anajulikana kwa kuwa kiongozi mnyenyekevu, mchapakazi, asiye na makasiriko, na mwenye maono ya maendeleo kwa wananchi wake wa Babati Vijijini na taifa kwa ujumla. Ameendelea kuwa mfano wa viongozi wanaochanganya utaalamu, uzalendo na utumishi uliotukuka kwa taifa.
Kwa uteuzi wake kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo ameandika ukurasa mpya wa historia ya Mkoa wa Manyara — akiungana na viongozi wachache kutoka mkoa huo waliowahi kushika nyadhifa za juu katika mihimili ya dola.



