*Awataka wawe tayari kuwezesha maendeleo, waende kwa gia ya kupandia mlima
*Amshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua_
WAZIRI MKUU, Mteule, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watumishi wa umma ambao ni wazembe, wala rushwa, wavivu na wazembe, wenye lugha mbaya kwa Wananchi wabadilike ili kuwezesha maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo yaweze kutimia.
“Watumishi wa umma na Watanzania wote tuwe tayari, lazima twende kwa gia ya kupandia mlima, lazima twende kwa gia ya kupita kwenye bahari yenye mawimbi, lazima twende kwa gia ya kupita kwenye anga lenye mawingu, lazima chombo kifike salama na watu wake wakiwa salama. Kwa watumishi wavivu, wazembe nitakuja na fyekeo na rato. Lazima maono ya Mheshimiwa Rais na ahadi ambazo amewaahidi Watanzania zitekelezwe.”
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 13, 2015) bungeni jijini Dodoma alipokuwa akitoa shukurani baada ya kuthibitishwa na Bunge kufuatia uteuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kwamba yote yaliyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchanguzi ya CCM ya 2025/2030 na yaliyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi yatatekelezwa iwapo wataendelea kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kudumisha amani.
“Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitano, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejitambulisha kuwa ni rais anayetaka matokeo ya haraka yanayotatua matatizo ya Watanzania. Amefanya hivyo wakati alipoingia madarakani kukiwa na tatizo kubwa la umeme aliweka jitihada kubwa za kukamilisha mradi mkubwa wa bwala la Mwalimu Nyerere ambalo limemaliza tatizo la kukatika katika kwa umeme.”
Kadhalika, Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani kulikuwa na tatizo la vifo vya akinamama wajawazito pamoja na watoto kutokana na upungufu wa hospitali na vituo vya afya. “Katika kipindi kifupi amejenga zaidi ya hospitali 119 za wilaya, zaidi ya vituo vya afya 649 katika kata mbalimbali, zaidi ya zahanati 2,800 nchi nzima.”
“…Katika kipindi kifupi amejenga shule mpya zaidi 2,700 za msingi na shule zaidi 1,300 za sekondari na madarasa zaidi 97,000, hivyo hivyo katika sekta zingine ikiwemo kununua CT Scan hospitali zote za mikoa na MRI katika hospitali za Kanda pamoja na mitambo ya kuchimbia visima vya maji kwenye kila mkoa na kila ukanda na hiki ndicho kilichowafanya Watanzania wamchague kwa wingi na nimetaja machache.”
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa dira mpya ya 2050, Dkt. Mwigulu amesema dira imebeba matumaini makubwa ya Watanzania wakiwemo vijana ambao ndio hasa walengwa hivyo kuna kazi kubwa ya kuanza utekelezaji wake pamoja na kumalizia viporo vya dira ya 2025.
“Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunipendekeza kushika nafasi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Natambua uzito wa majukumu haya pamoja na maratajio yake pamoja na matarajio ya Watanzania, nitafanya kazi kwa bidii, kwa uaminifu mkubwa na jiutihada kubwa kuweza kukidhi matarajio haya.” Dkt. Mwigulu amethibitishwa kwa kupata kura 369 kati ya kura 371 zilizopigwa.




