Na Meleka Kulwa – Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemthibitisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kikao kilichofanyika leo Novemba 13, 2025, katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma. Dkt. Nchemba aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Sita, amepata kura 369 za ndiyo kati ya kura 371 zilizopigwa na wabunge, huku kura mbili zikiharibika.
Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa, Dkt. Nchemba amesema kuwa Serikali anayoiongoza itakuwa ya wananchi wote na haitabagua mtu kwa misingi yoyote. Amesema kuwa kila Mtanzania atapata haki ya kusikilizwa katika ofisi za umma, akibainisha kuwa anatambua changamoto wanazopitia wananchi wa hali ya chini kutokana na uzoefu wake binafsi wa maisha magumu baada ya kumaliza chuo.
Amesema kuwa alishawahi kufanya kazi ya kubeba zege na matofali ili kujipatia kipato, na hivyo anaelewa maumivu ya vijana wasio na ajira. Ameahidi kwamba Serikali itatekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutengeneza ajira milioni nane kwa vijana nchini, kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Aidha, Dkt. Nchemba amebainisha kuwa utendaji wa Serikali utajikita katika kutatua matatizo ya wananchi kwa matokeo ya haraka, sambamba na kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Amesema kuwa dira hiyo imebeba matumaini makubwa kwa Watanzania, hasa vijana, na kwamba awamu hii ya pili ya Serikali ya Awamu ya Sita itaanza utekelezaji wake rasmi.
Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za kijamii kwa kuendeleza miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya Rais Samia, ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, vituo vya afya na miradi ya umeme vijijini.
Amesema kuwa hatua hizo ni kielelezo cha Serikali inayoweka kipaumbele katika maisha ya wananchi, huku akiahidi kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora katika maeneo yote ya nchi.
Pia,Dkt. Nchemba Amesema kuwa atasimamia kwa bidii, uaminifu na uwajibikaji mkubwa majukumu yake kama Waziri Mkuu, akisisitiza kuwa Serikali yake itakuwa ya ushirikiano, inayoweka mbele maslahi ya wananchi wote bila ubaguzi.



