Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akizungumza na Vijana wa Chama cha Skauti Tanzania (TSA) alipokuwa akifungua Kundi la Skauti katika Shule ya Sekondari ya Manguanjuki iliyopo Manispaa ya Singida Novemba 8, 2025. Kushoto ni Kamishna wa Skauti Wilaya ya Singida, Veronica Mwambuta na kulia ni Kamishna wa Skauti Wilaya ya Ikungi, Robert Michael.
………………………………….
Na Dotto Mwaibale, Singida
VIJANA nchini wametakiwa kutojihusisha na uvunjifu wa amani nchini badala yake wailinde kwa kufa na kupona kila kona ya nchi.
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa
wa Singida, Frederick Ndahani wakati
akizungumza na Vijana wa Chama cha Skauti Tanzania (TSA) alipokuwa akifungua Kundi la Skauti katika Shule ya Sekondari ya Manguanjuki iliyopo Manispaa ya Singida.
Ndahani alisema kuna baadhi ya vijana wameanza kuiga mitindo na mienendo
isiyo mizuri kutoka mataifa mengine, jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani
iliyojengwa kwa muda mrefu..
“Kila mtu ana uraia wake, na
sisi vijana wa Tanzania uraia wetu ni wa Kitanzania. Tunapaswa kuendelea kuilinda
amani ya nchi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo,” alisema Ndahani.
Aidha, aliwahimiza vijana wa
Skauti kutimiza ahadi zao kwa Mungu na Taifa kwa kuwa wazalendo, watiifu, na
walinzi wa amani na mali za umma.
Alisema ni jukumu la kila kijana
kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapoona dalili za
uvunjwaji wa amani au uharibifu wa mali za umma.
“Ni muhimu kwa kila kijana
kulinda mali za umma na hata mali za wawekezaji. Wengi wao wamewekeza nchini na
kuwaajiri vijana wengi. Tukiharibu amani, tunapunguza uwekezaji na kuathiri
utalii ambao ni chanzo cha mapato ya fedha za kigeni,” aliongeza Ndahani.
Kwa upande wake, Kamishina wa Skauti Wilaya ya Singida, Veronica Mwambuta, aliwataka wanachama wa Skauti
kutojihusisha na vitendo vya vurugu au uvunjwaji wa amani vinavyofanywa na
baadhi ya vijana nchini.
Naye Enetha Mathias,
mwanaskauti kutoka Shule ya Sekondari Manguanjuki, alisema wako tayari
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kufichua watu wenye nia ya
kuharibu amani.
Mathias aliitaka Serikali kuendelea kushirikiana na makundi yote ya
kijamii, ikiwemo wazee, vijana, viongozi wa dini na vyama vya siasa, ili
kudumisha maridhiano na kuendeleza amani ya nchi.
![]() |
| Kamishna wa Skauti Wilaya ya Ikungi, Robert Michael, akizungumza. |
Vijana wa Skauti wa shule hiyo wakiwa katika hafla hiyo.
Vijana wa Skauti wa shule hiyo wakiwa katika hafla hiyo.
Hafla hiyo ikifanyika.
Nidhamu na usikivu ukitamalaki kwenye hafla hiyo.
Kamishna wa Skauti Wilaya ya Ikungi, Robert Michael, akisisitiza jambo kwenye hafla hiyo. Kutoka kushoto ni Mratibu wa Uthibiti wa Maafa na Majanga, Skauti Mkoa wa Singia, Fatuma Ayubu, Kamishna wa Skauti Wilaya ya Singida, Veronica Mwambuta na Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani.
Wanafunzi wa shule hiyo waliojiunga na Skauti wakila kiapo.
Wanafunzi wa shule hiyo waliojiunga na Skauti. Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (katikati) na viongozi mbalimbali wa Skauti wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule hiyo.




