Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amemuapisha Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa mara ya pili katika Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hafla ya uapisho imefanyika leo, tarehe 08 Novemba 2025, Ikulu Zanzibar, na imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa dini, maafisa wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka SMZ na SMT, pamoja na wanafamilia.
Mara baada ya kuapishwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa katika kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Nane atahakikisha anasimamia vema utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na miradi yote ya maendeleo kwa maslahi mapana ya Wazanzibari.
Aidha, Mhe. Hemed amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano nchini.




