Mbunge Mteule wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Juma Zuber Homera,akizungumza na wananchi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi katika viwanja vya Ofisi ya CCM ya zamani Namtumbo mjini.
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Namtumbo, wakimsikiliza Mbunge Mteule wa Jimbo la Namtumbo Juma Zuber Homera(hayupo pichani)katika viwanja vya Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Namtumbo mjini
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya ya Namtumbo,wakimpongeza Mbunge Mteule wa Jimbo la Namtumbo Juma Zuber Homera kulia.
……….
Na Mwandishi Maalum, Namtumbo
MBUNGE Mteule wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma kupitia Chama cha Mapinduzi Dkt Juma Zuber Homera,amewaomba Wananchi na Viongozi wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kuungana pamoja ili kuijenga Wilaya yao kiuchumi,kijamii na maendeleo.
Homera,ametoa wito huo hivi karibuni, wakati anawashukuru Wanachama wa Chama cha Mapinduzi na wananchi baada ya kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi(INEC) kuwa mshindi wa nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Namtumbo.
Homera amepata kura 171,162 sawa na asilimia 99.78 akimshinda mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo Boniphasia Mapunda aliyepata kura 233 na Mgombea wa CUF Rashid Mfaume aliyepata kura 145.
Amewataka watu wenye uwezo wa kifedha na nafasi mbalimbali za uongozi, kuwasaidia wenzao wenye changamoto ili nao wapate fursa ya kushiriki vyema kwenye kazi za maendeleo na kuijenga Namtumbo yao.
Aidha Dkt Homera,amemshukuru Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpitisha kuwa mgombea wa Ubunge Jimbo la Namtumbo na Kamati ya Siasa Mkoa wa Ruvuma kwa kumuamini kupeperusha Bendera ya Chama hicho katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Homera,amesema atahakikisha anafanya kazi usiku na mchana katika kuwatumikia watu wa Namtumbo ambao kwa muda mrefu wamebaki nyuma kimaendeleo licha ya Wilaya hiyo kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo ardhi yenye rutuba.
“Namtumbo tujiandae kufanya kazi kwa mchaka mchaka hakuna kusimama wala kulala,mtumishi ambaye atashindwa kwenda na kasi tunayotaka atafute mahali pakwenda kufanyia kazi lakini sio hapa Namtumbo,tunahitaji maendeleo ya haraka kwani bado tuko nyuma ikilinganisha na Wilaya za wenzetu”alisema.
Homera,amehaidi kufuatilia mradi wa ujenzi wa Barabara ya Lumecha Wilayani Namtumbo hadi Kilosa kwa Mpepo Mkoa wa Morogoro ambayo kwa muda mrefu inatajwa kujengwa kwa kiwango cha lami lakini hadi sasa ujenzi wake bado haujaanza.
“Barabara hii ni ya kimkakati inayokwenda kuinua Uchumi na ipo kwenye ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi,mimi nitakwenda kusukuma ujenzi wake ili iweze kujengwa haraka”alisema Homera.
Homera ametaja barabara nyingine ambayo ni muhimu kwa wananchi ni Mtwarapachani-Lusewa-Nalasi hadi Tnduru mjini yenye urefu wa kilometa 330 ambayo imewekwa kwenye mpango wa lami.
Alisema,Barabara hiyo ni muhimu kwa Uchumi wa Wilaya ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma na itakapojengwa kwa kiwango cha lami itasaidia kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kati ya Namtumbo na Tunduru.
Ametaja mradi mwingine ambao atakwenda kusimamia utekelezi wake ni stendi ya mabasi,mradi wa maji safi na salama katika mji wa Namtumbo,miundombinu ya elimu,afya na kumaliza tatizo sugu la migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Amesema,atahakikisha anasimamia soko la Tumbaku kwa kuleta makampuni mengi zaidi kwa ajili ya kununua zao hilo ambalo ni nguzo kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na Wilaya hiyo ili wakulima waweze kunufaika kwa kupata fedha nyingi.
“Kwenye sekta ya kilimo,tutaanzisha kituo cha mauzo ya mbolea ili kuwaondolea wakulima usumbufu wa kwenda makao makuu ya Mkoa Songea mjini umbali wa kilometa 67 kwenda kununua pembejeo,tunaka wakulima wetu wapate pembejeo hapa hapa Namtumbo”alisema Homera.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Namtumbo Zuber Lihuwi,amewaomba wananchi wa Namtumbo kumuunga mkono Homera katika majukumu yake na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo itawezesha wananchi kujiongezea kipato na kuondokana na umaskini.
“Wananchi wa Namtumbo tusikubali tena kuendelea kuwa masikini,awamu hii tumepata mtu sahihi mwenye uchungu na sisi ambaye atakwenda kutuletea maendeleo tuliyoyahitaji kwa muda mrefu”alisema Lihuwi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Dkt Primus Nkwera,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi katika wilaya ya Namtumbo ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amewaomba wananchi,kuwa na imani kubwa na Dkt Homera kwani ni mtu sahihi,mzalendo,upendo na anapenda maendeleo ya wenzake ndiyo maana Chama cha Mapinduzi kimemchagua na kumsimamisha kuwa Mgombea Ubunge katika Jimbo la Namtumbo.



