Mbinga, Ruvuma
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mbinga imepokea jumla ya shilingi milioni 403,772,750.00 kutoka serikali kuu kwa ajili ya kurejesha mawasiliano ya barabara zilizoharibiwa na mvua za masika pamoja na tetemeko la ardhi lililotokea mwezi Mei, 2024.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga, Mhandisi Oscar Mussa, amesema kuwa fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi miwili mikubwa ya ukarabati wa barabara ambazo zilikuwa muhimu kwa wakazi wa maeneo husika.
“Katika kipindi cha masika tulikumbwa na madhira makubwa yaliyosababisha kuporomoka kwa udongo na kuharibu miundombinu ya barabara. Serikali ilitupatia shilingi milioni 283,172,000.00 kwa ajili ya kurudisha mawasiliano katika barabara ya Langilo kuelekea mkoha,” amesema Mhandisi Musa.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 7.2 inahudumia wakazi wa Kata ya Langilo, hususan kijiji cha Mkoha. Madhara makubwa yalitokea katika eneo la daraja la mto Makomba ambapo udongo uliporomoka na maeneo mengine yaliathiriwa na mawe yaliyoporomoka kwenye kona za barabara hiyo.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi Machi mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba na kuongeza kuwa kazi zilizokamilika hadi sasa ni pamoja na kurudisha tuta, kujenga mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa zaidi ya Km 1 na kuondoa mawe yaliyokuwa yameziba barabara.
Ametaja mradi wa pili ni ukarabati wa barabara ya Longa–Kipololo–Litoho, ambayo imepokea shilingi milioni 120,600,750.00 baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi. “Eneo la Kalavati la mto Ntunduwalo, hususani katika barabara ya Longa liliporomoka tuta, lakini kwa sasa barabara hiyo imefunguliwa na inapitika kwa usalama”.
Mhandisi Mussa ameishukuru serikali kwa kuwezesha kupata fedha hizo kwani wananchi wa Mbinga wanaendelea kutoa shukrani kwa uwezeshaji huu ambao umeleta nafuu katika usafiri na usafirishaji pamoja na uchumi wa maeneo husika,




