*Ataka biashara zifanyike kwa amani na kulinda ujirani mwema kati ya Tanzania na Kenya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amesisitiza umuhimu wa wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao Mpakani mwa Tanzania na Kenya kupitia kwenye Lango la Namanga kuendelea kulinda amani na kukuza ujirani mwema kati ya Mataifa hayo mawili yenye kujitegemea katika shughuli za kiuchumi na Kijamii.
Mhe. Makalla ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 06, 2025 alipokutana na Makundi ya wafanyabiashara ndogo ndogo na wasafirishaji wanaofanya biashara katika mpaka wa Namanga Wilayani Longido, alipofika kwaajili ya kukagua hali ya ulinzi na usalama na ufanyaji wa biashara katika eneo hilo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyeagiza shughuli zote za kiuchumi na Kijamii kurejea kawaida mara baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania.
“Mpaka wetu huu kwa wananchi mliopo hapa lazima mumshukuru Mungu kwa kuwa hapa kwasababu tunapata riziki kupitia shughuli zetu za biashara na Mpaka huu umegeuka kuwa tegemeo letu. Mpaka huu usipokuwa na usalama shughuli zote hapa zitatoweka, niwaombe muulinde mpaka huu ninyi wenyewe kwa kuhakikisha hakuna mtu anayekuja kuhatarisha amani hapa na muwe mabalozi wazuri wa amani.” Amesema CPA Makalla.
Katika maelezo yake, CPA Makalla amewataka wananchi hao wa pande zote mbili kuwa walinzi wa Mpaka huo pamoja na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za wanaohamasisha na kutenda vitendo vya uvunjifu wa amani, akiwataka kutokuwa na hofu na maafisa wa usalama wanaofanya shughuli zao za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao.




