Farida Mangube, Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amewashukuru wakazi wa Mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha kabla wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili cha awamu ya sita.
Mhe. Malima ametoa shukrani hizo leo, Novemba 4, 2025, ofisini kwake wakati wa mazungumzo na Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, Dkt. George A. Pindua, aliyefika kuzungumzia ratiba za ibada ya kumuingiza kazini, iliyokuwa imepangwa kufanyika Novemba 9, 2025, mkoani humo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa utulivu, amani na usalama vilivyoshuhudiwa katika Mkoa wa Morogoro kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ni matokeo ya ushirikiano wa wananchi wote, si juhudi za mtu mmoja pekee.
Aidha, Mhe. Malima amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuliongoza Taifa katika kipindi chote cha uchaguzi kwa kudumisha hali ya ulinzi na usalama, hatua iliyowawezesha Watanzania kurejea kwenye shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa amani.
Aidha Mhe. Malima amewashukuru viongozi wote wa dini wa madhehebu mbalimbali kwa mchango wao mkubwa wa kuhubiri amani, upendo na utulivu, na kumtaka Askofu huyo kufikisha salamu hizo kwa viongozi wenzake wa dini mkoani humo.
Pia, ametoa shukrani kwa makundi mbalimbali ikiwemo wazee, vijana, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na wanahabari kwa kusaidia kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kupiga kura kwa amani na utulivu.
Mhe. Malima hakuwasahau mama lishe, baba lishe, machifu wa kimila, wamachinga, asasi zisizo za kiserikali, madereva wa bodaboda, magari makubwa, mabasi, daladala na bajaji, akiwataka wote wapokee pongezi hizo kwa mchango wao katika kudumisha amani mkoani humo.
Vilevile, ameishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa, pamoja na watumishi wote wa umma na taasisi za Serikali kwa ushirikiano wao mkubwa.
Kwa upande wake, Askofu Mteule Dkt. George Pindua alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano anaouonesha tangu aingie madarakani, hususan katika kipindi cha maandalizi ya uchaguzi, ambapo aliwahusisha viongozi wa dini katika vikao vya maandalizi, hatua iliyochangia kuimarisha utulivu wa Mkoa




