NA DENIS MLOWE, IRINGA
MJUMBE Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Abri Asas, amepiga kura mapema leo katika Kituo cha Chuo cha Afya 1, Manispaa ya Iringa, na kueleza kuwa zoezi la kupiga kura limeanza kwa utulivu na amani kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupiga kura, Asas amesema kuwa yeye pamoja na wananchi wengine tayari wametimiza wajibu wao wa kikatiba na kusema kwa ufupi tumetiki na zoezi limeenda kwa amani na utulivu.
Salim Abri alisema kuwa hali ya utulivu na amani imetawala katika Manispaa ya Iringa na Mkoa kwa ujumla, jambo linalodhihirisha uimara wa demokrasia na umoja wa Watanzania kama ambavyo nilitoa taarifa wakati wa kufunga kampeni za Mafinga Mjini.
Aliongeza kuwa moja ya chaguzi ambazo zimefanyika mwaka huu zenye amani na utulivu hivyo kuwa miongoni mwa chaguzi zenye historia kubwa ya amani nchini tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, na anaamini utahitimishwa kwa mafanikio makubwa na utulivu wa kipekee.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, mara baada ya kumaliza haki yake ya kikatiba ya kupiga kura katika Kituo cha Kinondoni Flat 1 kilichoko kata ya Gangilonga amezungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa zoezi la kupiga kura limeanza vizuri huku wananchi wakijitokeza kwa wingi
Alisema hali ya usalama katika vituo vyote vya kupigia kura mkoani Iringa ni shwari na maandalizi yamekuwa mazuri, hivyo wananchi waendelee kujitokeza kutumia haki yao ya msingi.
Kheri James amesisitiza kuwa kura zitahesabiwa kwa usalama na matokeo kutangazwa kwa utulivu, huku akiwataka wananchi kuepuka vitendo au maneno vinavyoweza kuvuruga amani.
Alisema kuwa zoezi la kupiga limeanza kwa utulivu na litamalizika kama lilivyoanza kwa utulivu na amani hivyo watu waendelee kujitokeza kupiga kura bila kuhofia vurugu.
Aidha, amepongeza wananchi waliopiga kura mapema na kuwataka wengine kufuata mfano huo, akisisitiza kuwa muda bado unaruhusu ili kila mmoja atimize wajibu wake wa kikatiba wa kupiga kura kwa viongozi wanaowataka kuwaletea maendeleo.
Wakati huo huo mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa Iringa Zaina Mlawa majira ya saa 3 asubuhi amejitokeza kwenye kituo cha kupigia kura cha Idydc 2 cha kata ya Gangilonga kumchagua Rais pekee baada ya kubadilisha taarifa zake ambazo ni fomu namba 8.
Alisema kuwa awali alijiandikishia Bahi jijini Dodoma hivyo alipohamishiwa kikazi alibadilisha taarifa zake zinazoruhusu kupiga kura kwa nafasi ya Rais.
Mlawa alisema kuwa wanashukuru zoezi la kupiga kura linaendelea katika hali ya amani na utulivu hivyo wale ambao bado wafike kwenye vituo walivyopangiwa kupiga kura.
Naye Balozi Pindi Chana alikuwa mmoja ya wananchi waliofika mapema katika kituo cha Kupiga kura cha Chuo cha Afya 1 kupiga kura kwa ajili ya Rais na kusema kuwa anafurahishwa na amani na utulivu kwenye kituo hicho.
Aliwapongeza tume huru ya uchaguzi kwa kuwapa elimu nzuri wasimamizi wa chaguzi katika vituo na kusema kuwa zoezi limekuwa bora kabisa na wito ni mkubwa kwa wananchi.




