NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa, Ezekiel Wenje, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa amani na utulivu, kwani kufanya hivyo ni kutekeleza haki yao ya kikatiba.
Amesema hayo wakati wa ufungaji wa mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Oktoba 28, 2025, jijini Mwanza.
Amesema kuwa dhana ya “kazi na utu” ndiyo msingi wa haki za wananchi katika Katiba ya nchi, akibainisha kuwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa, ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Usaili inayomsaidia Rais kuteua wajumbe wa Tume ya Uchaguzi, ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
Aidha, amebainisha kuwa Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa haki ya kupiga kura ni haki ya kikatiba ya kila mtu binafsi, bila kujali chama anachokiunga mkono. Ameongeza kuwa yeye binafsi amekuwa ndani ya CHADEMA kwa miaka 15 akiwa mjumbe wa Kamati Kuu, hivyo anazungumza kwa uzoefu.
Amesema kuwa hakuna chama chochote cha siasa wala mtu yeyote aliyekwenda mahakamani kupinga uhalali wa uchaguzi huo, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kujitokeza kupiga kura kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Aidha, amesema kuwa uchaguzi ni mchakato unaoongozwa kwa mujibu wa sheria, na kwamba mageuzi yoyote yanayohitajika nchini yanafanyika kupitia vyombo halali kama Bunge, ambacho ndicho chenye mamlaka ya kutunga na kurekebisha sheria.
Amesema kuwa hoja za kisiasa hazitatuliwi mitaani, bali kupitia mijadala ya hoja bungeni ambako wabunge wa pande zote hushiriki kujenga hoja na kupitisha sheria.
Pia, amebainisha kuwa madai ya baadhi ya watu wanaodai kuwa Tanzania haina demokrasia hayana ukweli, kwani hakuna chama chochote cha siasa kilichozuiwa kushiriki uchaguzi. Amesema uchaguzi ni mchakato unaofuata taratibu na misingi ya kikatiba, na hivyo ni jukumu la Watanzania wote kushiriki ili kuimarisha demokrasia ya taifa.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 



                                
                             