Na Mwandishi wetu, Mirerani
MBUNGE mteule wa viti maalumu Mkoa wa Manyara kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Regina Ndege, amewataka wakazi wa eneo hilo, kujitokeza kwa wingi kupiga kura zote kwa mgombea urais wa chama hicho Dkt Samia Suluhu Hassan ili kumheshimisha kwani amefanikisha miradi mingi ya maendeleo.
Ndege akizungumza mji mdogo wa Mirerani kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni wilayani Simanjiro, amesema wana Manyara wana deni kubwa kwa Dkt Samia hivyo watalilipa kwa kura nyingi.
“Mama yetu ametupatia fedha nyingi za maendeleo wana Manyara ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji na mengine hivyo ni wakati wetu wa kumheshimisha kwa kumpa kura zote ndiyo,” amesema Ndege.
Hata hivyo, amewaomba wana Simanjiro kumpa kura nyingi za ndiyo mgombea ubunge James Ole Millya na wagombea udiwani wa kata zote 18 wa CCM.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro James Ole Millya amesema ana uhakika Dkt Samia atapata kura zote za ndiyo, yeye na wagombea udiwani wa CCM wa eneo hilo.
“Wana Simanjiro wamejiandaa vyema kupiga kura kwani nimetembelea kata zote 18 na kujionea hali ilivyo kwani wana CCM wana hamu ya kuonyesha ushindi kupitia kura za ndiyo,” amesema Ole Millya.
Aliyekuwa mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi.
“Wana Simanjiro, Manyara na watanzania kwa ujumla, watatiki kwa Dkt Samia kwa ajili ya maendeleo ya barabara za lami, madarasaya ya shule za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya na hospitali,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Ormemei Laizer amesema Simanjiro ni ya kijani na ngome ya CCM hivyo anategemea ushindi wa kishindo.
Kiria amewataka wananchi, hususan wanachama na wapenzi wa CCM, kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kumpa kura ya ndiyo mgombea urais Dkt. Samia, mgombea ubunge Ole Millya na madiwani wa kata 18.



