Na Meleka Kulwa -Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari (MB), amewataka wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka 18 kujitokeza kwa wingi kesho, tarehe 29 Oktoba 2025, katika vituo vyao vya kupigia kura ili kutumia haki yao ya kikatiba kwa kuchagua viongozi wanaowataka.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 28, 2025, katika Ukumbi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulipo Mtumba, Jijini Dodoma, Mhe. Hamza S. Johari Amesema kuwa kushiriki kupiga kura ni wajibu wa kikatiba na ni njia pekee ya wananchi kuamua mustakabali wa nchi yao kwa amani na demokrasia. Aidha, amesisitiza kuwa kila raia anapaswa kutambua umuhimu wa kura yake, kwani kupitia uchaguzi huo Serikali hupata mamlaka yake kutoka kwa wananchi kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 8(1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Mhe.Hamza Johari amebainisha kuwa Katiba hiyo imeweka utaratibu wa kufanyika kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kila baada ya miaka mitano, na kwamba uchaguzi wa kesho ni halali kwa mujibu wa masharti ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.
Aidha, amesema kuwa kwa sasa hakuna sababu yoyote ya kikatiba au kisheria inayoweza kuzuia au kusogeza mbele uchaguzi huo, akibainisha kuwa mawazo ya kutaka ucheleweshwe ni kinyume cha Katiba na hayapaswi kupewa nafasi.
Amesema kuwa wagombea wote wa nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani wamepatikana kwa mujibu wa Katiba na sheria, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa amani kutekeleza haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Mhe. Hamza Johari amesema kuwa Kifungu cha 129 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kinakataza vitendo vya matumizi ya nguvu, vitisho au hila yoyote vinavyolenga kumzuia mtu kupiga kura. Ameonya kuwa yeyote atakayefanya hivyo atakuwa anatenda kosa la ushawishi mbaya kwa mujibu wa sheria.
Aidha, amewataka wale wanaopanga kufanya maandamano, vurugu au kuzuia wananchi wengine kutumia haki yao ya kikatiba kuacha mara moja, akibainisha kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai na Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria.
Pia, Mhe. Johari amebainisha kuwa nchi inaongozwa kwa misingi ya Katiba na sheria, na kama Mshauri Mkuu wa Serikali katika masuala ya kisheria, ataendelea kusimamia utekelezaji wa Katiba na Sheria za nchi ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa lenye utawala wa sheria.



