NA JOHN BUKUKU
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Murida Mshota, amesema jijini Mwanza Oktoba 27, 2025 kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kura zote kutoka kwa wafugaji zinapigwa kwa wakati, ambapo ifikapo saa saba mchana Oktoba 29, watakuwa wametekeleza wajibu wao ukamilifu katika halmashauri zote 180 nchini.
Ametoa wito kwa vijana, hususan wafugaji, kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima na badala yake kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na kurudi majumbani kusubiri matokeo.
Amesema Serikali imefanya kazi kubwa, hivyo wananchi wanapaswa kuwapa zawadi ya kura viongozi waliotekeleza maendeleo hayo.
Aidha, amebainisha kuwa chama hicho kimeweka miundombinu ya mawasiliano katika maeneo yote ya wafugaji ili kuhakikisha ushiriki mkubwa katika zoezi la kupiga kura Oktoba 29, 2025.
Pia, amebainisha kuwa chama hicho kimesajili zaidi ya wafugaji milioni 4.268 nchi nzima.
Aidha, amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika sekta ya mifugo, ikiwemo kuongeza bajeti ya wizara hiyo hadi kufikia shilingi bilioni 475 kutoka bilioni 169 ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia, ameeleza kuwa kwa mwaka huu pekee Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 210 kwa ajili ya chanjo za ng’ombe na bilioni 69 kwa utekelezaji wa miradi mingine ya mifugo. Amesema pia kuwa Serikali imejenga zaidi ya majosho 754 katika halmashauri 184 nchini.
Mshota amesema kuwa mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,700 hadi kufikia tani milioni 14, jambo linaloonyesha mafanikio makubwa katika sekta hiyo.
Aidha, amebainisha kuwa zaidi ya wafugaji 8,313 wamepata mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 100.9, jambo ambalo awali halikuwepo kutokana na changamoto za ukosefu wa sifa za kukopa.
Kuhusu migogoro kati ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, Mshota amesema hali hiyo sasa imetoweka kufuatia uzinduzi wa mpango wa “Tuungane” uliofanywa na Rais Samia mkoani Morogoro, ambao umeleta umoja na amani miongoni mwa wananchi.



