Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi ambaye pia ni mgombea mwenza wa urais kupitia chama hicho, amesisitiza kuwa amani ni utajiri wa thamani kubwa kwa Taifa, akiwataka Watanzania wote kuilinda hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
Akizungumza leo Oktoba 27, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, kiongozi huyo amesema tukio la kupiga kura ni la kihistoria na ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kwa amani bila kufanya vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.
“Tukio la kupiga kura ni muhimu sana. Niwasihi wananchi wenzangu tukapige kura kwa amani. Amani ni utajiri wetu, tuvilinde vyombo vyote vya demokrasia na utulivu wetu kama Taifa,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Ameeleza kuwa kampeni za mwaka huu zimekuwa za kistaarabu na zenye usalama, jambo linaloonyesha uimara wa taasisi za kidemokrasia na usimamizi bora wa uchaguzi nchini.
Aidha, amempongeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha misingi ya demokrasia na kuhakikisha vyama vyote vinashiriki siasa kwa uadilifu na kwa usawa.
“Jaji Mutungi amekuwa mfano wa kuigwa katika kuendeleza demokrasia. Amekuwa mlezi mzuri wa wanasiasa nchini, akihakikisha kila chama kinapata nafasi sawa,” alisema.
Katibu Mkuu huyo pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uthabiti wake katika kuliongoza Taifa licha ya changamoto na upotoshaji unaojitokeza kwenye mitandao ya kijamii.
“Tunaona chokochoko nyingi mitandaoni, lakini tunampongeza Rais kwa msimamo wake. Ameendelea kusimamia nchi bila kupelekeshwa, jambo linalotupa matumaini makubwa kama Taifa,” aliongeza.
Akizungumzia ajenda kuu ya chama hicho, Katibu Mkuu alisema kuwa Agenda ya NCCR-Mageuzi ni maridhiano ya kitaifa, akibainisha kuwa chama hicho kimejikita katika kuhimiza umoja, mshikamano na ushirikiano wa Watanzania bila kujali tofauti za kisiasa.
“Kwa mwenendo huu wa amani, tuna imani kuwa mgombea yeyote atakayeshinda atatangazwa kihalali na kwa utulivu,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa chama hicho kinapinga maandamano yoyote ya kisiasa yanayoweza kuhatarisha amani, na badala yake kinaunga mkono “maandamano ya kwenda kupiga kura, si ya vurugu.”
Mwisho, Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuichagua NCCR-Mageuzi, akisema chama hicho ndicho suluhisho la maridhiano, umoja na maendeleo ya kweli ya Taifa.
“Niwaombe Watanzania, tujitokeze kwa wingi Oktoba 29. Tukiichagua NCCR, tumechagua maridhiano, umoja na mustakabali mwema wa Taifa letu,” alihitimisha.




