Baadhi ya viongozi wa Vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Dens Masanja wakati akifungua Mkutano wa wadau wa zao la Korosho wa Mkoa wa Ruvuma uliofanyika jana mjini Tunduru(Picha na Muhidin Amri)
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja,akifungua Mkutano wa wadao wa zao la korosho wa Mkoa wa Ruvuma uliofanyika jana mjini Tunduru,Mkoa wa Ruvuma katika msimu wa mauzo ya korosho 2025/2026 umepanga kukusanya na kuuza kilo 35,000,000(Picha na Muhidin Amri)
………..
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
MKOA wa Ruvuma,katika msimu wa mauzo ya zao la korosho 2025/ 2026 umepanga kukusanya zaidi ya tani 35,000 sawa na kilo 35,000,000 ikiwa ni ongezeko la kilo 3,391,962 zilizouzwa katika msimu wa kilimo 2024/2025.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas amesema hayo jana,katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja kwenye Mkutano wa Wadau wa zao la Korosho uliofanyika mjini Tunduru.
Brigedia Abbas alisema,takwimu za uzalishaji wa korosho zinaongezeka mwaka hadi mwaka kwani katika msimu 2024/2025 Mkoa huo ulizalisha kilo 31,608,038 zenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 93.14 ikiwa ni ongezeko la kilo 5,545,715 sawa na asilimia 58.38.
“katika msimu 2023/2024 wakulima wa Mkoa huo walifanikiwa kuzalisha jumla ya kilo 26,062,323 zenye thamani ya Sh.bilioni 45.5 huku bei ikiwa kati ya Sh.2,947 hadi 3,510 kwa kilo moja”alisema Abbas.
Alisema,zao la korosho ni kati ya mazao makuu ya kilimo katika mkoa wa Ruvuma lenye mchango mkubwa kimaendeleo na uchumi wa Mkoa,Taifa na mkulima mmoja mmoja na wakulima wengi wamefanikiwa kuboresha maisha yao na kujiletea maendeleo kupitia zao hilo.
Aidha alisema,Serikali imetoa kwa wakulima wa korosho viuatilifu bure na mabomba ya kupulizia kwa bei ya ruzuku kwa lengo la kuwapunguzia mzigo mkubwa wa kuhudumia mikorosho yao ili kuongeza tija.
“wakulima wamenufaika na utaratibu wa upatikanaji wa pembejeo za korosho ambapo kilo milioni 5,962,550 za Salfa ya unga imesambazwa,viuatilifu vya maji lita 270,573 na sumu ya kudhibiti wadudu lita 110,432 na zoezi la upokeaji limeanza Mwezi April 2024 na kumalizika mwezi Septemba 2025”alisema Abbas.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD)Marcelino Mrope alisema,uzalishaji wa zao la korosho katika Mkoa huo unaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na wadau wote kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya za hilo hasa upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za ugani.
Alisema,kuanzishwa na kusimamia kikamilifu mfumo wa stakabadhi ghalani umewezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei kubwa ambapo msimu uliopita bei ya korosho ilikuwa Sh.2.942.75 kwa kilo moja.
Alisema,mafanikio yaliyopatikana katika msimu 2024/2025 yametokana na maboresho ya sheria,kanuni na miongozo ya utekelezaji wa mfumo wa mauzo wa stakabadhi ghalani kwenye zao hilo.
Mrope,ameta baadhi ya mafaniko hayo ni kuongezeka kwa uzalishaji wa korosho ghafi,kuongezeka kwa ubora wa korosho ambapo korosho zote zilizozalishwa katika msimu huo zilikwa daraja la pili.
“Mheshimiwa mgeni rasmi,mafanikio mengine ni kuongezeka kwa wakulima wanaofungua akaunti za benki kwa ajili ya kupokea malipo kwani zaidi ya asilimia 98.5 wamefungua akaunti hivyo malipo yao kufanyika kwa wakati na wanalipwa ndani ya siku saba za kazi baada ya kufanyika kwa mnada”alisema Mrope.
Alisema,maandalizi ya msimu mpya huenda sambamba na vitendea kazi ikiwa ni pamoja na vifungashio,kamba,rangi,mizani,usafirishaji na maghala ya kuhifadhi korosho.
Alisema,TAMCU kwa kushirikiana na vyama vikuu vingine vinavyosimamia ukusanyaji wa zao la korosho wameunda kampuni ya pomoja(KCJE LTD) inayoratibu na kusimamia upatikanaji wa gunia ambapo wanahitaji gunia 437,500 na tayari wamepata gunia 600,000 zenye uwezo wa kuhifadhi korosho kilo 48,000,000.
Alisema,usambazaji wa gunia kwa vyama vya ushirika vya msingi ulianza tarehe 23 Oktoba 2025 na unafanyika kwa awamu kutokana na uzalishaji wa korosho na katika awamu ya kwanza tayari wamesambaza gunia 250,000 kwa Amcos 43 kati ya 53 zilizopo Mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani ya Njombe na Mbeya.
Mwenyeki wa TAMCU Mussa Manjaule,amevipongeza vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)kwa kusimamia zoezi la ukusanyaji wa korosho katika msimu wa kilimo 2024/2025 licha ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu.



