………
Hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2025 Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ilikuwa imekamilisha ujenzi wa minara 741 kati ya minara 758 iliyopangwa kujengwa katika kata 713 nchini. Mradi ambao unalenga kunufaisha vijiji 1,407 ambavyo awali havikuwa na huduma za mawasiliano, ambapo hadi sasa takribani vijiji 1,300 tayari vimefikishiwa huduma.
Serikali imetoa shilingi bilioni 126, ikiwa ni ruzuku kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu, unaotekelezwa kwa kushirikiana na makampuni ya simu. Juhudi hizi zimewezesha wananchi kupata huduma za kidijitali kwa urahisi, kuboresha maisha yao na kuongeza fursa za kiuchumi katika maeneo husika.
Minara 741 ambayo imekamilika, tayari imewashwa na inatoa huduma kwa wananchi, hizi ni jitihada endelevu za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na maendeleo ya kiteknolojia na mawasiliano, hususan walioko vijijini na pembezoni.




