Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbagala kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Sheikh Said Kinyogoli, ameahidi kupigania maslahi ya wananchi wa jimbo hilo endapo atachaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa muda wa maneno umeisha na sasa ni wakati wa matendo.
Akizungumza wakati wa kufunga kampeni zake za ubunge zilizofanyika jana katika eneo la Mbagala Kijichi, Kinyogoli alisema wananchi wa jimbo hilo wanahitaji kiongozi jasiri atakayesimama kuwawakilisha kwa sauti bungeni, badala ya wabunge wanaokaa kimya bila kuchangia hoja muhimu.
“Jimbo letu lazima lipate mtu wa kulipigia kelele ili tupone. Tunaambiwa elimu bure, lakini wazazi bado wanachangia hadi mishahara ya walimu. Mwaka huu hatucheki na yeyote, tunataka ushindi ili tuiseme Mbagala yetu,” alisema Kinyogoli huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Aidha, Kinyogoli aliwataka wananchi kuachana na ushabiki wa vyama na badala yake kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kuwatumikia kwa vitendo.
“Sasa hivi hatuhitaji ushabiki wa vyama, tunahitaji mtu atakayetusaidia na kutusemea. Nichagueni mimi Kinyogoli, ili Mbagala iwe jimbo la mfano ambalo wengine watakuja kujifunza,” aliongeza.
Katika mkutano huo, Kinyogoli pia aliwaahidi waendesha bodaboda kuwa ndani ya miezi mitano baada ya kuchaguliwa, hakuna atakayekamatwa kwa kukosa leseni, kwani atahakikisha kila dereva anapata leseni. Aliahidi pia kujenga kituo maalumu cha vijana kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi na kubadilisha mitazamo yao kuhusu ajira na maendeleo.
Kwa upande wake, Katibu wa CUF Jimbo la Mbagala, Ibrahim Bakonzi, alisema chama hicho kimeendesha kampeni zake kwa amani tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipotangaza ratiba, na kwamba wamepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wa Mbagala.
“Tumefanya kampeni vizuri kwa njia zote, na wote wanamuunga mkono Said Kinyogoli. Hata baadhi ya viongozi wa CCM wameonyesha wazi kutambua uwezo wake. Kazi imeisha, tunasubiri ushindi,” alisema Bakonzi.
Bakonzi alimshukuru mgombea huyo kwa kujitolea muda na rasilimali zake katika kuhakikisha anasimamia maslahi ya wananchi, huku akimkumbusha kuwa ana deni kubwa kwa wananchi kutokana na upendo waliomwonyesha tangu mwanzo wa kampeni.
Wakati huo huo, mgombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni kupitia CUF, Wakili Msomi Mohamed Majaliwa, amewataka wananchi wa Kigamboni kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani, akisema hakuna sababu ya vurugu au maandamano.
“Kazi tumeshaimaliza. Jitokezeni mpige kura kwa amani. Wabunge hatutaki kuongoza walemavu wa kujitakia; kazi yetu ni moja tu — kupiga kura na kusubiri matokeo,” alisema Majaliwa.
Akihitimisha, Bakonzi aliliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha ulinzi wa watu na mali katika vituo vya kupigia kura, akisisitiza kuwa haki itawale wakati wa kutangaza matokeo.
“Tunawaomba polisi wasimamie haki itendeke. Mgombea atakayeshindwa atangazwe kwa haki. Mkikataa, tutalazimika kudai haki hiyo,” alisema Bakonzi.




