Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais wa Shelisheli, Dr. Patrick Herminie, baada ya kuapishwa kua Rais wa awamu ya sita wa nchi hiyo, katika tafrija ya uapisho iliyofanyika katika hoteli ya Story Seychelles, jijini Victoria Sychelles, Oktoba 26. 2025 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Rais wa Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Patrick Herminie mara baada ya kuapishwa na akatumia nafasi hiyo kuwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema leo (Jumatatu, Oktoba 27, 2025) kwamba katika mambo ya msingi ambayo Rais Dkt. Samia alitaka yawasilishwe ni uhakika wa Tanzania kuendelea kuiunga mkono Jamhuri ya Shelisheli na kuwapongeza wananchi wake kwa uamuzi walioufanya kupitia uchaguzi wao wa kidemokrasia na kuwawezesha kumpata Rais mpya.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alitaka pia nimhakikishie Rais Dkt. Herminie kwamba Tanzania itaendelea kufanya kazi na Shelisheili ikiwa ni kuunga mkono jitihada za waasisi wa mataifa haya kuendeleza ushirikiano kwenye nyanja za uchumi, ulinzi, siasa, biashara na uwekezaji.”
Amesema Rais wa Shelisheli ameridhia kuanzishwa kwa Tume ya Ushirikiano ya Pamoja (JPC) itakayotoa fursa kwa watalaamu wa nchi hizo mbili kukutana na kuratibu kwa pamoja masuala kutoka kwenye sekta na wajadili kwa kina mahitaji ya mahusiano kutoka nchi hizi mbili. “Tuna mahusiano katika wizara za elimu, afya, ulinzi na kibiashata hasa usafirishaji wa anga na utalii.
Amesema kauli ya Rais mpya wa Shelisheli imeleta matumaini kwamba Tanzania sasa imepata rafiki ambaye atahuisha mahusiano ambayo yalikuwepo hapo awali. “Rais huyu ameleta mwelekeo mpya alipozungumzia kuwa chama chake kilikuwa na urafiki wa muda mrefu na Chama cha Mapinduzi.
Hivyo tunaamini chama chake cha United Seychelles (US) kitaimarisha mahusiano na Chama cha Mapinduzi na kufanya vyama vyetu kuwa imara.”
Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt. Herminie ambaye aliapishwa jana kuwa Rais wa sita wa nchi hiyo, alishawahi kuwa Spika wa Bunge la Seychelles na alishafanya ziara kadhaa nchini miaka ya nyuma. Hivyo anaielewa Tanzania kwa ubora na umahiri wake katika masuala mbalimbali.
Mapema, Waziri Mkuu alikutana sekretarieti ya wanadiaspora wa Shelisheli ambao walimweleza fursa zaidi za uwekezaji zilizomo nchini humo hasa katika maeneo ya utalii, ajira kwenye sekta za afya, elimu, kilimo cha bustani na waongoza utalii.
Amewataka wazingatie taratibu na sheria za nchi waliyomo lakini pia waendelee kutafuta fursa za kuisaidia Tanzania ili nchi yao iweze kunufaika. Amewataka kila inapopatikana fursa watoe taarifa nyumbani ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka.
Naye, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Cosato Chumi aliwahakikishia viongozi hao wa diaspora kuwa Serikali imesikia ushauri na maoni waliyoyatoa na itayafanyia kazi kwa haraka huku akimpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo amekuwa akishughulikia hoja mbalimbali zinazotolewa na wanadiaspora.
“Binafsi nimeambatana na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika nchi nyingi na kote huko amekuwa akitatua changamoto zinazojitokeza na kukwamua mambo yaliyokuwa yamekwama kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwenye mikataba ya ushirikiano baina ya Tanzania na Belarus, Nigeria na Ghana,” alisema.
Katika ziara hiyo ya siku moja, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Cosato Chumi; Balozi wa Tanzania nchini Kenya anayeiwakilisha Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Bernard Kibesse na maafisa waandamizi wa Serikali.



