Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, leo tarehe 26 Oktoba 2025, amempokea aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati Bw. Jackson Jingu, aliyehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa Kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida.
Kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Singida na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, ambaye pia ni mratibu wa kampeni za CCM Kanda ya kati, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa.
Akizungumza mara baada ya kujiunga na CCM, Ndugu Jackson Jingu, amewaasa wananchi kutoshiriki katika uvunjifu wa amani wala maandamano kwa kuwa wanaotoa wito wa maandamano hawatoshiriki na wengine hawatokuwepo nchini. Amesema utoaji wa matamko yanayoashiria uvunjifu wa amani yanayotolewa na baadhi ya vyama vya siasa yanapaswa kukemewa ili kulinda amani ya nchi




