Na Meleka Kulwa- Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule amewasisitiza waandishi wa habari kuwatoa hofu wananchi kwa kuwaeleza kuwa mkoa upo salama na serikali imejipanga kuhakikisha wanakuwa salama na mali zao wakati wa mchakato mzima wa zoezi la upigaji Kura
Pia, ameviomba vyombo vya habari kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na kudumisha amani wakati wa kipindi cha uchaguzi na baada ya Uchaguzi
Senyaamule ameyasema hayo Oktoba 24,2025 wakati wa kikao na waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma ili kujadili maendeleo ya mkoa wa Dooma katika kipindi cha miaka minne pamoja na kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
“Vyombo vya habari tusaidieni kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki zoezi la kupiga kura na tuendelee kuwaelimisha juu ya amani wakati huu wa uchaguzi kwa mkoa wetu wa Dodoma na nchi kwa ujumla,” amesema Bi. Senyamule.
Aidha, amewaomba waandishi wa habari kuwatoa hofu wananchi wa Dodoma kwa kuwaeleza kuwa mkoa huo upo salama na serikali imejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi.
“Mkoa wa Dodoma upo salama, wananchi wajitokeze kupiga kura. Serikali imejipanga kuhakikisha kila mahali panakuwa salama,” amesema.
Bi. Senyamule amesema kuwa waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi, akibainisha kuwa mwaka 2020 kiwango cha wananchi waliojitokeza kupiga kura kilikuwa chini katika Mkoa wa Dodoma.
“Mwaka huu, ajenda ya ziada tuliyoiongelea ni ile ya kimkakati kitaifa kuhusu uchaguzi wa Serikali Kuu. Ajenda muhimu ni kuhakikisha amani na utulivu wakati wa uchaguzi na kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura,” amesema Bi. Senyamule.
Amebainisha kuwa kikao hicho ni mwendelezo wa mazungumzo ya kila mwaka kati ya serikali na vyombo vya habari, vinavyolenga kutoa fursa ya kusikiliza maoni, kero na mapendekezo ya wananchi pamoja na kutoa taarifa za maendeleo ya mkoa.
Aidha, Bi. Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma umeendelea kuona mabadiliko makubwa katika sekta ya miundombinu, ikiwemo ujenzi na upanuzi wa barabara mbalimbali.
Amebainisha kuwa barabara kutoka Chamwino kuelekea Msalato na Uwanja wa Ndege zinapanuliwa, barabara za kilomita kumi kuelekea Iringa na Singida zinaongezwa, na barabara ya mzunguko wa ndani ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji. Aidha, upembuzi yakinifu wa ujenzi wa treni ya ndani umekamilika, huku mpango wa kujenga Chuo Kikubwa cha TEHAMA (ICT) Afrika ukiwa KImepangwa kujengwa kwenye eneo la hekari 200.




