Na Meleka Kulwa -Dodoma
Viongozi wa dini kutoka mikoa ya Dodoma na Singida wamekutana jijini Dodoma katika kongamano la kuliombea taifa amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kongamano hilo limefanyika Oktoba 25,2025, katika Hotel ya Morena Jijini Dodoma, kongamano Hilo lililikuwa linaongozwa na kaulimbiu isemayo “Amani na Utulivu ni Jukumu Letu” na limewakutanisha viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali walioungana kwa sauti moja kuhimiza wananchi kudumisha amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Akizungumza katika kongamano hilo, Shekhe wa Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Viongozi wa Dini mbalimbali Mkoa wa Dodoma, ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, Alhaj Dkt. Rajab Mustafa Shabani, amesema kuwa ni muhimu kwa kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujitokeza kupiga kura kwani kufanya hivyo ni kutimiza haki ya msingi.
Aidha, amebainisha kuwa maandiko ya dini, ikiwemo Injili na Qur’an, yamehimiza kudumisha amani na utulivu pamoja na kushiriki katika masuala ya msingi ya kitaifa kama kupiga kura. Ameongeza kuwa maombi ni silaha kubwa ya kuilinda nchi dhidi ya maangamizo na adhabu, akitolea mfano aya ya 77 katika Suratul Furqan, inayozungumzia umuhimu wa maombi kwa Mwenyezi Mungu.
Amesema kuwa maombi yanaweza hata kubadilisha kadhia ya Mungu, na kwamba dua, sala na maombi ni nguzo muhimu za kuimarisha amani na baraka za taifa.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwa wasikivu na watiifu kwa maelekezo ya viongozi wa serikali na kuyatekeleza kwa mujibu wa sheria, pamoja na kuyaheshimu maelekezo ya viongozi wa dini katika mambo ya msingi yanayozingatia taratibu na mafundisho ya dini zao.
Kwa upande wake, Shekhe wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro alitoa alitoa wito kwa viongozi wa dini kujitathmini na kuepuka kuwa chanzo cha migawanyiko katika jamii.
“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kujiingiza kwenye maneno ya kisiasa na kuilaumu serikali kwa mambo ambayo wao wenyewe wanachangia kuyafanya tumeshuhudia siku za hivi karibuni viongozi wa dini wakijiteka wenyewe na kusingizia serikali,hivyo turejee kwenye misingi ya imani ya upendo, ukweli na amani,” amesema Shekhe Issa.
Kongamano hilo, lililojumuisha viongozi wa Kiislamu, Kikristo na madhehebu mengine, liliambatana na maombi maalum kwa ajili ya taifa, likiwa na ujumbe wa umoja na mshikamano bila kujali tofauti za imani au itikadi za kisiasa.







