Na Mwandishi Wetu TPA, Morogoro
Michezo ya 18 ya Bandari (InterPort Games 2025) imehitimishwa rasmi mjini Morogoro kwa shamrashamra, nidhamu ya hali ya juu na ushindani uliovutia, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Wakili Plasduce Mbossa, alisisitiza umuhimu wa watumishi wote wa sekta ya bandari kushiriki kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Hotuba ya kufunga michezo hiyo ilisomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TPA, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Bw. Mbarakiwa Masinga, katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, watumishi wa sekta ya bandari, vyama vya wafanyakazi, wanamichezo na wananchi wa mkoa huo.
Katika hotuba yake, Wakili Mbossa aliipongeza kamati ya maandalizi kwa ubunifu, nidhamu na uwajibikaji uliowezesha michezo hiyo kufanyika kwa mafanikio makubwa, huku akiwashukuru washiriki wote kwa kushindana kwa amani na kuonesha mfano wa uzalendo, mshikamano na ushirikiano wa kweli wa kikazi.
“Michezo ya Bandari imekuwa jukwaa muhimu sana la kuimarisha afya za watumishi wetu, kuongeza tija kazini na kudumisha undugu wa taasisi zinazohusiana na shughuli za bandari nchini,” alisema Mbossa kupitia hotuba yake.
Ameongeza kuwa michezo hiyo si burudani pekee bali ni nguzo muhimu katika kujenga afya bora, kuimarisha ufanisi wa kazi na kuleta mshikamano wa kitaifa miongoni mwa wafanyakazi wa sekta hiyo nyeti.
Kauli mbiu ya mwaka huu, “Michezo ya Bandari 2025 kwa Afya, Tija na Mshikamano kwa Wafanyakazi Tujitokeze Kupiga Kura Oktoba 29,” imetafsiriwa na washiriki kama wito wa kizalendo unaochanganya michezo na wajibu wa kiraia katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
ZPC Yatamba, Dar na Tanga Zang’ara
Mashindano ya mwaka huu yalimalizika kwa matokeo ya kuvutia katika michezo mbalimbali, ambapo timu ya Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) iliibuka bingwa wa mpira wa miguu baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Bandari ya Dar es Salaam katika mchezo wa fainali uliosisimua mamia ya mashabiki mjini Morogoro.
Kwa upande wa netiboli, ZPC iliendelea kutawala baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 16 dhidi ya Bandari ya Dar es Salaam, ikionesha ubora na kasi katika mchezo huo.
Bandari ya Tanga nayo iliweka historia kwa kutwaa ubingwa wa mpira wa kikapu, huku Bandari ya Dar es Salaam ikiwakilisha vyema kwa kuibuka mabingwa wa mpira wa wavu kwa wanaume na wanawake.
Michezo mingine iliyopambanua vipaji ni pamoja na kuvuta kamba, riadha, bao, drafti, karata na mpira wa wavu, ambayo yote yalileta ushindani mkubwa kati ya taasisi shiriki.
Afya, Tija na Mshikamano Nguzo za Mafanikio
Bw. Masinga alisema mashindano hayo yamekuwa zaidi ya michezo kwani yamejenga afya bora kwa watumishi, kuimarisha nidhamu ya kikazi, na kukuza ari ya kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa ndani ya taasisi za bandari.
“Tunajivunia kuwa mashindano haya yamefanyika kwa amani, kwa ushirikiano mkubwa na kwa nidhamu ya hali ya juu. Hii ni dalili kwamba sekta ya bandari ina watumishi wenye uzalendo na dhamira ya dhati ya kulitumikia taifa,” alisema Bw. Masinga.
Aliongeza kuwa TPA itaendelea kuwekeza katika michezo na afya za watumishi wake, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo kuhakikisha watumishi wake wanakuwa wenye nguvu, ari na morali ya kazi.
Morogoro Yatajwa Kitovu Kipya cha Michezo ya Bandari
Michezo ya mwaka huu imehudhuriwa na washiriki zaidi ya 600 kutoka TPA Makao Makuu na bandari zake za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Kigoma na Mwanza, pamoja na washiriki kutoka ZPC, TASHICO, na DP World Dar es Salaam Ltd.
Wakazi wa Morogoro wametajwa kuwa mfano wa ukarimu, kwa mapokezi mazuri na ushirikiano mkubwa uliochangia kufanikisha mashindano hayo yaliyodumu kwa zaidi ya wiki moja.
“Morogoro imeonesha kuwa ni kitovu kipya cha michezo ya Bandari nchini. Watu wamejitokeza kwa wingi, mazingira ni rafiki, na ari ya michezo imekuwa kubwa kuliko miaka iliyopita,” alisema mmoja wa waandaaji wa michezo hiyo.
Katika hotuba yake, Wakili Mbossa alihitimisha kwa kutoa wito kwa watumishi wote wa sekta ya bandari na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa amani na utulivu kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, akisisitiza kwamba hiyo ni sehemu ya uzalendo na uadilifu wa kiraia.
“Tuendelee kushirikiana, tushikamane kama familia moja ya bandari, na tuendelee kuwatumikia Watanzania kwa moyo wa uzalendo, uaminifu na uadilifu mkubwa,” alihitimisha Mbossa.
Michezo ya Bandari (InterPorts Games) imekuwa sehemu muhimu ya kalenda ya TPA kwa miaka 18 sasa, ikilenga kujenga umoja, kukuza afya, kutambua vipaji na kuimarisha ushirikiano wa kikazi kati ya taasisi zote zinazohusiana na shughuli za bandari nchini Tanzania Bara na Zanzibar.




