NA DENIS MLOWE, IRINGA
BAADA ya mafanikio makubwa ya tamasha la Land Rover lilofanyika jijini Arusha, Klabu ya Land Rover nchini inatarajia kufanya tamasha hilo mkoani Iringa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na baadhi ya maeneo ya Utalii mkoani hapa.
Tamasha la Land Rover Iringa 2025 litakuwa mara ya kwanza kufanyika mkoani hapa na kushirikisha wamiliki zaidi ya 500 waliokubali kushiriki tamasha hilo mkoani hapa.
Akizungumza kuhusu tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta alisema kuwa kitendo cha klabu ya Land Rover nchini kuleta tamasha hilo ni kuchochea Utalii ndani ya mkoa wa Iringa na wamejipanga vyema kuweza kufanikisha tamasha hilo.
Alisema kuwa kwa mkoa wa Iringa tamasha hilo limeandaliwa na Klabu ya Land Rover kwa kushirikiana ofisi ya chama cha watalii, wizara ya utalii na Tanapa hivyo wanapongezwa kwa kuweza kuleta mkoani hapa.
Sitta amewakaribisha watu wote kushiriki tamasha hilo kwani licha ya kufanyika mkoani hapa lakini litawashirikisha watu kutoka mataifa mbalimbali kwahiyo wanatarajia magari zaidi ya 500 hii ni fursa ya kibiashara na Iringa na vivutio zaidi ya 34 ambavyo vitatangazwa.
Alisema kuwa hadi sasa wameanisha maeneo mawili kwa ajili ya wageni ambapo eneo la kwanza ni River Valley Camp site na Kihesa Kilolo kwa ajili ya kulala kutokana watu wengi wanapenda mazingira ya asili kuweka tent zao za kulala.
Alisema kuwa eneo la Kihesa Kilolo ndio liltatumika watu kukusanyika na msafara utaanza pale na kuelekea Samora na siku ya tarehe 30 msafara utaelekea Ruaha Nationa Park.
Sitta aliongeza kuwa watatumia tamasha hilo kutangaza vivutio vya utalii mkoani hapa na Iringa itachangamka siku hizo na fursa kwa wananchi kufanya biashara.
Alisema kuwa licha ya Tamasha hilo klabu ya Land Rover itatumia muda huo kutoa msaada kwa jamii ambapo kamati itaamua ni eneo gani litaguswa.
Vilevile alisema wale ambao watapenda kushiriki tamasha hilo basi wanaruhusiwa na wafike ofisi za mkuu wa wilaya na kisha wataunganishwa na klabu ya Land Rover nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi Klabu ya Land Rover nchini , Augustine Namfua alisema kuwa tamasha la Land Rover Iringa lina lengo la kukuza utalii eneo husika na litafanyika ipasavyo kutembelea vivutio ambavyo bado havijajulikana sana na vile vinavyojulikana.
Alisema kuwa tamasha la Land Rover lina matukio makubwa mawili ambapo kuna maandamano au msafiri wa magari ya Land Rover na kusisimua uchumi wa eneo husika ambapo kutakuwa na sehemu ambayo wakazi wa Iringa watapata fursa ya kufanya biashara kwa wale wajasiriamali wadogo baada ya kukusanyika katika uwanja wa Samora mji utapata fursa ya kupokea wageni mbalimbali ambao watanunua vitu mbalimbali.
“Matarajio yetu ni kufikisha magari 500 ambayo yatakuja na watu ambao wanaweza fika 1000 katika tamasha hilo hilo hivyo wanakaribishwa sana kwenye tamasha na fursa kwa wafanyabiashara wote wa malazi vyakula ni muda mwafaka wa kujiandaa.
Namfua alisema wanakaribishwa watu wote wenye Land Rover mkoani hapa kushiriki tamasha hilo ambalo linarajiwa kufanyika Novemba 28 hadi 30 mwaka huu.



