Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Mkoa wa Manyara R.C Queen Cuthbert Sendiga amewataka wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite, kuhakikisha wanafanya shughuli zao za uchimbaji kwa kuzuia na kupunguza athari za magonjwa ya kifua kikuu na silikosesi na kuhakikisha wanatekeleza uwajibikaji kwa jamii (CSR).
RC Sendiga ameyasema hayo wakati akizungumza na wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Mazubu Grand Hotel mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.
Ameeleza kwamba wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite wanatakiwa kuangalia afya na usalama wa wafanyakazi wao pindi wakiwa migodini.
“Kanuni za afya migodini mzifuate ili kuondokana na vumbi kwani hivi karibuni nimekwenda hospitali ya Kibong’oto hali siyo nzuri kwa wagonjwa wachimbaji niliowakuta huko,” amesema RC Sendiga.
Pia, amewaasa wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kutekeleza takwa la kisheria la utekelezaji wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwani halijafanyiwa kazi ipasavyo.
Amesema siyo vyema kwa wachimbaji madini kutoshiriki CSR kwani inakuwa aibu kwake pindi akiwa kwenye mikutano ya kitaifa makao makuu ya nchi, jijjini Dodoma.
Hata hivyo, RC Sendiga ameteua kamati maalum na kuongeza wachimbaji madini watano kwa ajili ya kusimamia suala zima la afya ya wachimbaji madini ya Tanzanite.
Majina ya wachimbaji hao watano watakaokuwa kwenye kamati hiyo itakayokuwa chini ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mwalimu Fakii Raphael Lulandala itaongozwa na Mwenyekiti wa MAREMA, Elisha Nelson Mnyawi.
Wajumbe wengine ni Katibu mkuu wa MAREMA Tariq Kibwe, Katibu msaidizi MAREMA Dkt Curtis Msosa, Makamu Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani, Peter Laizer na mjumbe wa MAREMA Shamym Babu Premsing.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi akisoma taarifa kwa RC Sendiga amesema hivi karibuni wametembelea wagonjwa wenye changamoto ya kifua kikuu na silikosesi katika hospitali ya Kibong’oto.
Elisha ameeleza kwamba walipofika katika hospitali hiyo ya Kibong’oto wamebaini kuna wagonjwa 41 walio na kifua kikuu ni 22 na changamoto ya kupumua silikosesi ni 19.
Ameeleza kwamba katika kuhakikisha wanapambana na vumbi kampuni ya God Charity wanakisima ndani ya ukuta chenye uwezo wa kutoa lita 100,000 kwa saa hivyo wataalam wakakikague ili wachimbaji wavute maji.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mwalimu Fakii Raphael Lulandala, amewataka wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite, wawe wanafika wenyewe pindi wakihitajika kuliko kutuma wawakilishi.
“Nawapongeza mmejitokeza kwa wingi kwenye kikao hili cha Mhe RC wetu wa Manyara, ila wengine wenye tabia ya kutuma wawakilishi muachane na hayo mazoea kwani mnahitajika ninyi wenyewe na siyo mwakilishi,” amesema DC Lulandala.



