Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbagala kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Kakulu Buchard Kakulu
……………
NA JOHN BUKUKU – TEMEKE
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbagala kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Kakulu Buchard Kakulu, amesema wananchi wa Mbagala wameshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, ambapo mradi wa mabasi yaendayo kasi (BRT) umekamilika na sasa wananchi wanafika mjini kwa dakika ishirini.
Amesema hayo Oktoba 23, 2025, katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye Uwanja wa Tanesco Buza, wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam.
Aidha, amebainisha kuwa katika sekta ya afya, serikali imekamilisha upanuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Zakhem na kujenga vituo vitatu vya afya katika kata za Tuangoma na Kibondemaji, jambo lililosaidia kupunguza adha ya wakazi wa Mbagala kufuata huduma mbali kama Temeke na Muhimbili.
Amesema kuwa katika sekta ya elimu, serikali kupitia uongozi wa Dkt. Samia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 16 kwa ajili ya miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule ya ghorofa katika mtaa wa Manga, huku katika sekta ya maji ikitolewa zaidi ya shilingi bilioni 3.9 kutatua changamoto za upatikanaji wa maji safi.
Amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna maeneo yanayohitaji ufuatiliaji, ikiwemo barabara ya Rangitatu kuelekea Kongowe yenye urefu wa kilometa 3.8, ambayo ipo kwenye Ilani ya CCM. Ameomba uongozi wa chama na serikali kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha, amebainisha kuwa serikali inaendelea kutandaza mtandao wa bomba la maji kutoka Kibada hadi Uhasibu na lingine kutoka Kisarawe hadi Tuangoma, miradi ambayo iko katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Pia amesema kuwa katika kata jirani kuna mfereji muhimu ambao umeingizwa katika Ilani na utatekelezwa baada ya uchaguzi.
Amesema kuwa wananchi wa Mbagala wamejipanga kuhakikisha wanampigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wote wa CCM katika nafasi za ubunge na udiwani.
Pia amesema kuwa CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao, na kwamba wananchi wa Mbagala wataendelea kuwa sehemu ya ushindi huo.