NA JOHN BUKUKU – TEMEKE
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema siasa safi ni kuhakikisha nchi inabaki salama, watu wake wako katika hali ya amani na kushirikishwa katika kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya TANESCO, Vituka, wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam, Dkt. Samia alisema msingi wa siasa safi ni ushirikiano, umoja na kujenga maridhiano miongoni mwa Watanzania bila kujali tofauti za kisiasa.
“Siasa safi ni pale tunapokaa pamoja, kuzungumza na kukubaliana kwa pamoja. Huo ndiyo ustawi wa taifa. Haya ndiyo mafundisho ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na serikali zimekuwa zikiendeleza misingi hiyo kwa nyakati tofauti,” alisema Dkt. Samia.
Aliongeza kuwa wakati wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Miaka 25 ijayo, Serikali ya Awamu ya Sita ilihakikisha inakusanya maoni ya wananchi na kuyatilia maanani katika utekelezaji wake, ikiwa ni sehemu ya kujenga taifa lenye ushirikishwaji wa kweli.
Dkt. Samia aliwataka vijana wa Tanzania kutokubali kudanganywa na watu wanaotaka kuharibu amani, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi salama na yenye fursa nyingi za maendeleo. “Vijana wangu, hii nchi ni yenu. Msiharibu amani tuliyonayo, fuateni katiba na sheria, mtaishi kwa furaha,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vipo macho kuhakikisha uchaguzi mkuu utafanyika kwa amani na utulivu, huku akiwataka wananchi wote waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 29, 2025.
“Mama yupo macho, vyombo vyenu vya ulinzi vipo macho. Hakutakuwa na changamoto yoyote.
Njooni mpige kura kwa amani,” alisema Dkt. Samia akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.