Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mgombea Ubunge wa Jimbo ka Kisarawe Dkt. Selemani Jafo.
……………..
NA JOHN. BUKUKU- BUZA TEMEKE
Mgombea Ubunge wa Jimbo ka Kisarawe Dkt. Selemani Jafo, akizungumza katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizofanyika Oktoba 23, 2025 katika viwanja vya TANESCO Buza, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, amesema kuwa Dkt. Samia ni kiongozi mwenye umahiri mkubwa katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, hususan katika sekta ya viwanda na biashara.
Amesema kuwa kabla ya juhudi za serikali inayoongozwa na Dkt. Samia, viwanda vingi vilikuwa vinashindwa kufanya kazi kutokana na changamoto ya upatikanaji wa umeme, hali iliyosababisha baadhi ya vijana kupoteza ajira. Amebainisha kuwa serikali imefanikiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme katika gridi ya taifa kufikia megawati 990 kupitia mradi wa Bwawa la Nyerere, hatua iliyosaidia kufufua viwanda vingi na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Aidha, amebainisha kuwa moja ya changamoto kubwa nchini ilikuwa ni upungufu wa sukari, ambapo mahitaji ya taifa ni tani 802,000 huku uzalishaji ukiwa tani 470,000. Amesema kuwa serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa sukari unaongezeka, ikiwemo kuanzisha viwanda vipya na kuimarisha vile vilivyopo.
Amesema kuwa serikali imeongeza uzalishaji wa mazao ya nafaka kutoka tani milioni 7 hadi milioni 14, hatua iliyotokana na sera bora za kilimo na uwezeshaji kwa wakulima. Amesema kuwa awali baadhi ya wafanyabiashara kutoka nje walikuwa wananunua mazao mashambani kwa bei isiyokuwa rafiki kwa wakulima wa ndani, jambo lililosababisha serikali kutoa maelekezo kuhusu biashara 14 zinazolenga kulinda maslahi ya wafanyabiashara wa Tanzania.
Aidha, amebainisha kuwa serikali imeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda nchini, ambapo awamu ya kwanza ya mpango wa “Mama Viwanda” inahusisha ujenzi wa viwanda nane vikubwa, kati ya hivyo, viwanda takribani milioni 6.5 vinatoa ajira kwa Watanzania, zaidi ya milioni moja wakiwa vijana.
Amesema kuwa katika Mkoa wa Kigoma, serikali imewekeza katika mradi wa umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma wenye urefu wa zaidi ya kilomita 620, hatua inayolenga kuboresha huduma ya umeme na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya ukanda huo.
Aidha, amewataka Watanzania kumuenzi na kumuunga mkono Dkt. Samia kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.